Kisa rasimu ya katiba, wanachama Simba wawaka

Muktasari:

  • Kamati hiyo ilisema rasimu hiyo imepata baraka ya serikali, lakini Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro akiwa nje ya nchi alinukuliwa akikataa juu ya jambo hilo, huku baadhi ya wanachama waliozungumza na Mwanaspoti leo mchana walisema kuna tatizo katika rasimu hiyo.

KLABU ya Simba inatarajiwa kufanya Mkutano Mkuu Jumapili, huku baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wakionekana kugawanyika juu ya rasimu ya katiba inayotarajiwa kujadiliwa na kupitishwa, ikiwa ni siku moja tu, tangu Kamati ya Maboresho ya Katiba ya Simba kutangaza imepata baraka zote za serikali.

Kamati hiyo ilisema rasimu hiyo imepata baraka ya serikali, lakini Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro akiwa nje ya nchi alinukuliwa akikataa juu ya jambo hilo, huku baadhi ya wanachama waliozungumza na Mwanaspoti leo mchana walisema kuna tatizo katika rasimu hiyo.

Wanachama hao wa Simba, wameingiwa na hofu na kuwagawa wakidai huenda isikidhi mahitaji ya klabu hiyo, huku Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage akitoa angalizo kwa mkutano wa Jumapili akisema ni vyema ungefanywa wa kawaida kisha ndipo uitishwe mkutano wa kujadili katiba hiyo.

Simba itafanya mkutano maalumu jijini Dar es Salaam ukiwa na ajenda mbalimbali ikiwamo ya kujadili na kupitisha rasimu hiyo mpya itakayorahisisha mchakato wa klabu hiyo kuendeshwa kwa mfumo wa hisa baada ya awali kukwama kutokana na katiba iliyopo kuwa na dosari.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wakili Hussein Kitta alitangaza kupitishwa kwa rasimu hiyo huku akielezea kesho kwenye mkutano mkuu wanachama watajadili na kuitolea mapendekezo iwe ipitishwe ama irekekebishwe tena kukidhi mahitaji ya klabu hiyo inayoachana na mfumo wa kumulikiwa na wanachama.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa Simba waliliambia Mwanaspoti kutokuwa na imani na kamati hiyo kwa madai ya kutozingatia mambo ya msingi yakayaisaidia klabu kupata nafanikio na kuinuka kiuchumi zaidi, licha ya kuwasilisha mapendekezo, ni kama yamepuuzwa ili kuubeba upande wa mwekezaji na sio klabu.

Wanachama hao walisema wamepata na kuipitia rasimu hiyo kabla ya kuingia kwenye mkutano  wa kesho, lakini bado wanaona ina upungufu, huku baadhi wakienda mbali kupinga kupitishwa wakitaka irekebishwe kwa masilahi mapema ya klabu ya Simba.

Mwanachama wa Simba ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema, anaenda kupinga rasimu hiyo, kwani haijazingatia mambo muhimu ambayo ni ya maendeleo kwa Simba.

"Nimeipata rasimu na nimeipitia vizuri yote, ila nataka kusema naenda kuipinga mkutanoni, kwani haijazingatia mambo ya msingi yatakayotuvusha hapa tulipo na kutupeleka sehemu nzuri zaidi," alisema Kaburu na kuongeza;

"Kwanza FCC walituelekeza Katiba ielezee uwepo kwa klabu na uhai wake. Tulitegemea klabu iwe na uhai wa malengo na madhumuni yatakayobeba uongozi, lakini sasa haielezi kitu kama hicho kwa maana nafasi ya mwenyekiti inabaki kuwa mjumbe tu."

Mweka Hazina wa Tawi la Simba Roho Mbaya, Daudi Simba alisema; "Kiukweli kwenye huo mkutano ndo kila kitu kitajulikana ila kuna mambo hayajawekwa wazi na binafsi sikubaliani nayo kama hili la nafasi ya Mwenyekiti bado halisema kazi yake ni ipi.

"Ukiisoma hii rasimu bado nguvu kubwa ipo kwenye Bodi ya Wakurugenzi na sio wanachama ambao ndio wenye klabu, tuna nia njema na tunahitaji misingi bora ya klabu kwa ajili ya kizazi chetu kama tulivyoikuta sisi, Mwenyekiti bado anaonekana kuwa mjumbe tu katika bodi jambo ambalo sio sahihi," alisema Simba na kuongeza;

"Haya mambo mengine yanapaswa kufanywa kwa weledi na kuzingitia nini klabu itanufaika nacho na sio kuangalia masilahi binafsi, wanachama nao ifike mahala tusimame na tusikubali kuendeshwa na vikundi vichache vya watu kutoa maamuzi makubwa kama haya kwenye kitu chetu."

Kwa upande wa Katibu wa Tawi la Wekundu wa Terminal, Justine Joel, alikuwa tofauti na wengine akisema ameifurahia rasimu hiyo kwa vile imezingatia mambo muhimu hasa kuondoa kifungu cha ukomo wa wanachama ambao awali ilikuwa kila tawi liwe na wanachama 50 lakini sasa hakuna kikomo.

"Sisi tuna wanachama zaidi ya 100 walio hai, lakini hili likipitishwa naamini tutafika hata 500 ni jambo zuri na nimeipitia rasimu kila kitu naona kipo sawa na Jumapili tutamaliza salama, na wale ambao hawajaipitia basi siku zilizobaki wafanye hivyo kuondoa maswali," alisema Justine

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Evodi Kyando akifafanua juu ya kupitisha rasimu hiyo alisema Simba waliipeleka kwao na waliiangalia na kubaini haina mambo yaliyo kinyume na kanuni na sheria ya za nchi na michezo na kuwaruhusu kwenda nayo kwenye mkutano.

"Tumekuwa tukikutana na viongozi wa Simba mara kadhaa kupitia BMT na Wizara husika, lengo sio kuwaambia wafanye nini katika Katiba yao, bali pale tunapoona mambo yapo kimya nasi tunaulizwa ndipo tunawatafuta kujua nini kinaendelea," alisema Kyando na kuongeza;

"Hivyo huwa tunataka watuambie wamefikia wapi, kikubwa ni kuona hawakiuki sheria na kanuni serikali, kazi yetu ni kuwaulizia na kama ni kinyume tunawaelekeza kwani serikali haitengenezi Katiba za klabu. Simba walipaswa kufanya mkutano Desemba mwaka jana walikuja kutuambia, wasogeze mbele kwani kuna mambo hayakukamilika.

"Mikutano hiyo ikumbukwe ni lazima sisi tuipitishe, tulikubali. Na hawawezi kufanya mkutano bila Katiba ndio maana wameleta rasimu yao kwetu nimeiangalia kama haina mambo ambayo ni kinyume na sheria, kanuni na serikali, nimeona iko sawa nimewaruhusu.

"Lakini kuwaruhusu huko hakumaanishi kwamba Katiba imekamilika, wanaenda kuijadili kama kutakuwepo na mapendekezo yao watakayoyaongeza wataongeza wataileta tena kwangu niipitie, nikiona ipo kinyume sitaipitisha na nitawataka wairekebishe tena," alisema msajili huyo.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria wa Simba, Hussein Kita alipotafutwa kuzungumzia baadhi ya mambo yaliyozungumzwa na wanachama, kuwa hayajawekwa katika rasimu hiyo alisema; "Ni kweli tulipokea maoni mengi sana kutoka kwa wanachama wetu na kweli hayajawekwa yote, ila hiyo haimaanishi kwamba mlango wa maboresho ya Katiba umefungwa.

"Sasa hivi tulianza na mambo ya msingi ambayo ni ya haraka ili tuweze kukamilisha mchakato wa Mabadiliko ya Mfumo wa uendeshaji wa klabu ambao umekwama kwa muda mrefu, hivyo maboresho ya Katiba yanaweza kufanyika tena na tena.

"Na kitu alichotueleza Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Damas Ndumaro ni kwamba turekebishe vifungo vilivyo kinyume na sheria na kanuni ya serikali, ambavyo kweli tulikuwa kinyume navyo na si kwamba serikali inasimamia Katiba," alisema Kita

Kwa upande wa Ismail Aden Rage, mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo alisema kwa namna mkanganyiko ulivyojitokeza kwa sasa ni vyema mkutano wa kesho, ungetumika kujadili mambo mengi kati ya ajenda zilizopo na wanachama wangeunda kamati huru ambayo ni ya wanachama na sio wajumbe wa bodi, ili iendeshe mchakato kisha baada ya siku 90 ndipo ufanyike mkutano wa kuijadili kwa kina na kuipitisha.

"Katiba haiwezi kujadiliwa na kupitishwa katika mkutano kama huu, hekima itumike na wanachama wote wakubaliane tu, ili utolewe muda kwa kamati huru ya wanachama kuichakata kisha irudishwe katika mkutano baada ya miezi mitatu. Duniani kote katiba huwa na mkutano maalumu wake na sio kama huo wa kesho, alisema Rage.

Simba ipo kwenye mchakato wa kuiendesha kwa mfumo wa hisa na ilishamtangaza Mohammed Dewji kama mwekezaji, anayeelezwa kawekeza Sh 20 Bilioni akimiliki hisa za asilimia 49 na 51 zinabaki kwa wanachama, japo mchakato mzima haujakamilika kwa sababu mbalimbali ikiwamo ishu ya dosari za katiba ya sasa.