KRFA yafunguka sababu kumdhamini Karia TFF

Muktasari:
- Akizungumza leo, Juni 20,2025 mjini Moshi, Mwenyekiti wa KRFA, Isaac Munis maarufu kwa jina la ‘Gaga’ amesema wamemdhamini Karia kwa kuzingatia kazi aliyoifanya katika kipindi cha miaka minane aliyokaa madarakani.
WAKATI harakati za uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zikipama moto, Chama cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), kimempa baraka mgombea urais Wallace Karia kuendelea na kipindi kingine cha uongozi.
Akizungumza leo, Juni 20,2025 mjini Moshi, Mwenyekiti wa KRFA, Isaac Munis maarufu kwa jina la ‘Gaga’ amesema wamemdhamini Karia kwa kuzingatia kazi aliyoifanya katika kipindi cha miaka minane aliyokaa madarakani.
“Niliona habari zinaendelea mitandaoni, waandishi wakanipigia simu kuniuliza kuhusu kumpa mtu mwingine endorsement (udhamini). Mmoja alipiga mpaka mara tano,” amesema Munis.
Akaongeza: “Tukaona si vyema kuendelea kuwa kimya ndiyo maana nikaitisha kamati ya utendaji na wajumbe wa mkutano mkuu. Tumeamua rasmi kumuidhinisha Karia. Siyo sisi tu, hata mkutano wa KRFA uliofanyika Januari ulilizungumzia hili.”
Munis amefichua kuwa hoja ya Karia kuendelea na uongozi ilianzia kwenye Mkutano Mkuu wa TFF Desemba 21, 2024 uliofanyika Moshi, ambapo Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alitoa wazo hilo na kuungwa mkono na Rais wa Yanga, Hersi Said.
“Sasa kama viongozi wa klabu kubwa kama Simba na Yanga waliunga mkono hadharani kwa nini sisi tusimpe tena nafasi? Mbona watu wanafahamu kazi alizofanya Karia. Huyu mtu mwingine wanayesema tumpe endorsement hata jina lake silijui. Nimelisoma tu mtandaoni,” amesema Munis.
Akiongeza kwa kwa utani amesema: “Tuweke wazi, kwa nini tutumie photocopy wakati original ipo na inafanya kazi vizuri?”
Mgombea wa nafasi hiyo, Shija Richard amesikika akilalamikia changamoto ya kukosa udhamini kutoka kwa wajumbe wa mkutano mkuu ambapo leo wakati akirudisha fomu, amesema anakusudia kufungua mashtaka kwenye kamati mbili za TFF - ile ya maadili na ya rufani ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF hadi sasa Karia amerudisha fomu ya kugombea nafasi ya urais akifuatiwa na Dk Mshindo Msolla, Shija na Ally Mayay waliorejesha leo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Agosti 16, mwaka huu ambapo nafasi saba zitawaniwa katika uchaguzi mkuu wa TFF ikiwemo ya urais na sita za ujumbe wa kamati ya utendaji.