Kealey anawindwa na timu England

Muktasari:
- Tetesi zinaeleza viongozi wa QPR wanafanya maboresho kwenye kikosi hicho kilichomaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi na imefungua mazungumzo na nyota huyo mwenye uraia wa nchini mbili Tanzania na Australia.
QPR FC inayoshiriki Ligi ya Champioship ya England inadaiwa imeanza mazungumzo na beki wa kulia mwenye asili ya Tanzania, Kealey Adamson anayekipiga Macarthur FC ya Australia.
Tetesi zinaeleza viongozi wa QPR wanafanya maboresho kwenye kikosi hicho kilichomaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi na imefungua mazungumzo na nyota huyo mwenye uraia wa nchini mbili Tanzania na Australia.
Juni 30 mkataba wa nyota huyo na Macarthur FC unaishia ukingoni, hata hivyo inaelezwa bado hajasaini mkataba mpya na klabu hiyo.
QPR FC inaamini kumpata beki huyo mwenye miaka 22 watakuwa wamelamba dume kutokana na uwezo mkubwa wa kukaba na kushambulia.
Macarthur alicheza kwa misimu miwili akitokea Sydney lakini msimu uliopita ulikuwa wa mafaniko zaidi kwake kutokana na kiwango bora alichoonyesha.
Msimu 2024–25, Kealey alicheza mechi 26 kwa jumla ya dakika 2,177 akifunga mabao mawili na kutoa pasi tatu za kufungia.
Kwa mujibu wa Fotmob, Kealey kwa kila mechi ana asilimia 88 ya kugusa mipira, mashambulizi asilimia 87, wastani wa kuzuia asilimia 85 na uwezo wa kuishinda mipira ya juu 78.
Takwimu hizo zinaonyesha nyota huyo alipata wastani wa alama 7.2 kila mechi kiwango ambacho ni cha juu hasa kwa beki wa pembeni na kuwa mmoja wa nyota wanaozungumzwa Australia.
Kumbukumbu nzuri kwa beki huyo ilikuwa Februari 06, Macurthur walipocheza na Western Sydney Wanderers licha ya kupoteza mabao 2-1 lakini alionyesha kiwango bora kiasi cha kumkaba nyota wa zamani wa Chelsea na Man United, Juan Mata anayekipiga katika kikosi hicho.
Machi mwaka huu baada ya ligi kutamatika Adamson aliteuliwa kama mshindi wa Macarthur Medal, tuzo anayopewa mchezaji bora wa msimu ndani ya klabu ikiwa ni ishara njema ya ubora na mchango wake kwa timu.