Kazimoto, Kiiza, Mgosi kubadilishana

Kocha wa Simba, Dylan Kerr.
Muktasari:
Kerr amesema mastraika Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Hamis Kiiza hawatakiwi kucheza katika eneo moja pekee kwani safu yote ya ushambuliaji inawahusu na wana uhuru wa kutembea kokote kuhakikisha wanafunga mabao.
KOCHA wa Simba, Dlyan Kerr, ametamka kuwa nyota wake watatu wanaocheza eneo la ushambuliaji wana kazi maalumu ya kubadilishana nafasi kuhakikisha timu hiyo inapata mabao na si kung’ang’ania nafasi moja.
Kerr amesema mastraika Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Hamis Kiiza hawatakiwi kucheza katika eneo moja pekee kwani safu yote ya ushambuliaji inawahusu na wana uhuru wa kutembea kokote kuhakikisha wanafunga mabao.
Mbali na hao, Kerr alisema nyota mwingine mwenye uhuru huo ni Mwinyi Kazimoto ambaye pia anaruhusiwa kuhaha kila kona kuhakikisha anapiga pasi makini za mabao kwa mastraika hao.
“Ninaposema wanacheza mastraika wawili mbele simaanishi wakae sehemu moja, wanatakiwa kutembea eneo lote la ushambuliaji kuhakikisha wanapata mabao.
“Kama wanahama kwenda pembeni wanatakiwa kukumbuka kuwa jukumu lao ni kufunga, wanatakiwa kurejea katikati na kufunga mabao,” alisema Kerr.
“Waige mfano kwa mastraika wa kimataifa, mtazame Lionel Messi, ni straika lakini anahama kwenda kila upande, akipata mpira anarejea katikati, nataka wacheze hivyo.”
Wakati huo huo kocha huyo Kerr ameonekana kuwa hataki mzaha kabisa baada ya kuwapiga mkwara viungo wake wote kama wanataka kupata nafasi katika kikosi chake wahakikishe wanaacha kabisa tabia ya kupiga pasi za nyuma.
Kocha huyo raia wa Uingereza alisema hapendi aina ya viungo ambao kila wakipata mpira wanarejesha nyuma wakati timu inatakiwa kusonga mbele na kutengeneza mashambulizi.
Kocha huyo alifichua siri kuwa kabla ya pambano lao la Simba Day dhidi ya Sports Villa ya Uganda, alikaa na kuzungumza na viungo wake akiwemo mfungaji wa bao pekee la mechi hiyo, Awadhi Juma na kumtaka ahakikishe timu inakwenda mbele kwa mbele na siyo kurudisha mipira nyuma.
“Kiungo anapata mpira anataka kurejesha nyuma wakati mbele kuna mchezaji yupo huru, beki wa pembeni naye unakuta tayari amepanda, hiyo tabia kwangu haina nafasi.
“Kabla ya mechi na Villa niliongea na Awadhi na wachezaji wengine pia, nilimwambia akiingia uwanjani ahakikishe timu inakwenda mbele, akipiga pasi za nyuma atakuwa hapati nafasi tena, naona alinisikiliza,” alisema Kerr