Kaseke: Pamba Jiji mechi moja tu freshi

Muktasari:
- Pamba iliyorejea katika Ligi Kuu baada ya kuisotea kwa miaka 23 tangu iliposhuka mwaka 2001, kwa sasa ipo nafasi ya 12 ikimiliki pointi 30 kupitia mechi 28 na imesaliwa kuvaana na JKT Tanzania na KMC kufunga msimu ikipambana kuepuka kuangukia katika play-off ya kushuka daraja.
KIUNGO mshambuliaji wa Pamba Jiji, Deus Kaseke amesema kwa hali ilivyo kwa timu hiyo inahitaji ushindi wa mechi moja tu kati ya mbili ilizonazo ili kubaki Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
Pamba iliyorejea katika Ligi Kuu baada ya kuisotea kwa miaka 23 tangu iliposhuka mwaka 2001, kwa sasa ipo nafasi ya 12 ikimiliki pointi 30 kupitia mechi 28 na imesaliwa kuvaana na JKT Tanzania na KMC kufunga msimu ikipambana kuepuka kuangukia katika play-off ya kushuka daraja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaseke aliyetua katika timu hiyo kupitia dirisha dogo la usajili la Januari mwaka huu, alisema kwa sasa macho na masikio ya timu kwa ujumla viko katika mechi hizo mbili muhimu, lakini faida waliyonayo ni kwamba wanahitaji pointi tatu kujiweka salama zaidi.
Kaseke aliyewahi kutamba na Mbeya City aliyopanda nayo daraja kwa mara ya kwanza kisha kupita Yanga na Singida Big Stars, alisema faida kubwa zaidi kwa Pamba Jiji ni kucheza mechi zote za mwisho nyumbani na hesabu zao washinde zote, japo hata moja kwa itakuwa freshi tu.
“Sisi kama wachezaji tunataka kushinda mechi moja kati ya mbili zilizobaki ili kujiweka pazuri kwa msimu ujao wa Ligi Kuu, kila mtu ana lengo la kuibakisha Pamba katika ligi.” alisema Kaseke.
“Tunataka kusalia Ligi Kuu, hivyo tutapambana kufa kupona kuhakikisha tunachukua pointi tatu.”
Kaseke alisema kwa kipindi hiki cha mapumziko kwa wachezaji wanapumzisha mwili, lakini akiendelea kujinoa vyema na kutuliza akili kabla ya kurejea na kukamilisha mipango yao.