Wakenya waifuata Simba Zanzibar kuipa sapoti, waitabiria kubeba kombe

Muktasari:
- Mchezo huo wa marudiano utafanyika kuanzia saa 10:00 jioni huku Simba ikiingia uwanjani ikiwa na deni la mabao 2-0 iliyoruhusu ugenini, huku ikihitaji ushindi wa 3-0 kubeba ubingwa.
Mombasa: BAADHI ya viongozi na mashabiki wa soka kutoka Kenya, wameanza safari ya kwenda Zanzibar kuisapoti Simba ambayo kesho Jumapili itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Jumapili.
Mchezo huo wa marudiano utafanyika kuanzia saa 10:00 jioni huku Simba ikiingia uwanjani ikiwa na deni la mabao 2-0 iliyoruhusu ugenini, huku ikihitaji ushindi wa 3-0 kubeba ubingwa.
Wakiwa katika shauku kubwa ya kushuhudia fainali hiyo, wameeleza matarajio yao kurudi wakiwa na furaha ya Simba kuibuka washindi wa kombe hilo.
Mmoja wa viongozi wa soka wa Kanda ya Pwani aliyethibitisha kwenda Zanzibar kushuhudia fainali hiyo ni Gabriel Mghendi.
“Nitafika Zanzibar kuiona mechi hiyo nikiitakia Simba ushindi ili iwe timu ya pili Afrika Mashariki baada ya Gor Mahia 1978 kuibuka mabingwa wa kombe hilo. Ushindi wao utaweza kuthibitisha kuwa hali ya soka ya kanda hii inazidi kuimarika,” amesema Mghendi, mwakilishi wa Pwani katika Kamati Kuu ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) akikumbushia ushindi wa Gor Mahia ya Kenya iliyotwaa Kombe la Washindi mwaka 1978 kabla ya michuano hiyo mwaka 2004 kuunganishwa na Kombe la CAF ndipo ikazaliwa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Joseph Kioko ambaye ni shabiki wa soka kutoka Changamwe jijini Mombasa aliyefuatana na wenzake watatu wakielekea Zanzibar wakipitia Dar es Salaam, amesema: “Tunakwenda Zanzibar kushuhudia Simba ikiunguruma na kuwashinda Waarabu Jumapili.”
Muamir Said wa Malindi, amesema ametoka Kenya jana Ijumaa asubuhi kuelekea Dar es Salaam ili leo Jumamosi apande meli kwenda Zanzibar kwa ajili ya kuishuhudia mechi hiyo ya kihistoria.
“Nimekuwa shabiki wa Simba kwa miaka mingi, nataka niishuhudie mwenyewe fainali yao,” amesema Said.
Sherry Maganga wa Taveta, amesema safari yake kutoka Kenya ni ya usafiri wa basi akipitia Arusha, kisha Dar es Salaam na kupanda meli kwenda Zanzibar.
“Napenda kushuhudia soka la Tanzania linavyovutia mashabiki wengi. Nimekuwa shabiki wa Simba na nitafurahia kuishuhudia mwenyewe ikishinda fainali kwani ushindi wao ni wa kujivunia sote Afrika Mashariki,” amesema Maganga.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Kaunti ya Mombasa (MCFA), Juma Goshi Ally, amesema kama mechi hiyo ingefanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, basi angefika kuishuhudia lakini Zanzibar ni safari ndefu hivyo hatawahi kufika.
“Ningependa sana kufika huko kushuhudia wawakilishi wetu Simba SC wakipigania hadhi ya soka la Afrika Mashariki lakini Zanzibar ni mbali sana, sitoweza kufika. Lakini naiombea Simba ushindi kwani ushindi wao utaipa kanda yetu sifa kubwa," amesema.
Mbali na hilo, taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya zinabainisha kwamba vibanda na kumbi za starehe zitaonyesha mechi hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu.