Ambokile aitega Mbeya City

Muktasari:
- Ambokile aliliambia Mwanaspoti kuwa mkataba wake unaisha, hivyo hana uhakika kama ataendelea kubaki Mbeya City kwani anaangalia sehemu yenye maslahi na mpira ndio kazi yake.
STRAIKA wa Mbeya City, Eliud Ambokile amesema pamoja na kufanikiwa kuirejesha timu hiyo katika Ligi Kuu, bado hana uhakika wa kuendelea kuwepo kikosini humo, huku akichekelea rekodi aliyoiweka katika Championship.
Ambokile aliliambia Mwanaspoti kuwa mkataba wake unaisha, hivyo hana uhakika kama ataendelea kubaki Mbeya City kwani anaangalia sehemu yenye maslahi na mpira ndio kazi yake.
Mbeya City imerejea Ligi Kuu baada ya kupotea misimu miwili nyuma ikiungana na Mtibwa Sugar ambayo ilishuka daraja msimu uliopita na sasa zinajipanga upya kwa ajili ya msimu ujao.
Ambokile alisema, licha ya ushindani waliokutana nao, mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na kuisha kwa matokeo ya bila kufunga na ile dhidi ya Biashara United ya sare ya 1-1, hawezi kuzisahau.
Alisema mechi hizo zilikuwa na matokeo ya kuwapa mwelekeo mzuri wa kupanda daraja, lakini walijikuta wakiendelea kusubiri hadi mechi tatu za mwisho.
“Ile mechi na Mtibwa Sugar nilikosa penalti mbele ya mashabiki wengi Sokoine, ilitupa presha mno, Biashara United tulitangulia wakasawazisha ikatupa ugumu kujipanga ila mechi dhidi ya Polisi Tanzania na Geita Gold ndio zilirejesha matumaini,” alisema Ambokile.
Straika huyo aliongeza kuwa mbali na kupandisha timu, anajivunia rekodi ya kwanza kufikisha idadi ya mabao 15 katika historia ya kazi yake ya soka akieleza kuwa hali hiyo imeongeza ari na morali kwake.
Kuhusu kubaki au kutimka kikosini humo msimu ujao, staa huyo aliyewahi kukipiga TP Mazembe ya DR Congo, amesema hana uhakika kwakuwa anasubiri ofa kutoka popote kutegemeana na maslahi.
“Msimu wa 2018/19 niliishia mabao 14, msimu huu ndio nimefikisha jumla ya mabao 15 (pamoja na matatu ya Kombe la Shirikisho) ikiwa ni mara yangu ya kwanza kufikisha idadi hii ya mabao katika maisha yangu ya soka la ushindani. Kwakuwa mpira ndio kazi yangu, popote pale nipo tayari kutoa huduma,” alisema straika huyo aliyemaliza Ligi ya Championship akiwa na mabao 12.