Kaseke aitanguliza Singida Big Stars

Thursday August 04 2022
kaseke pic
By Damian Masyenene

TIMU ya Singida Big Stars imekwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya wageni wao, Zanaco FC ya Zambia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Mchezo huo unapigwa kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida ukiwa ni sehemu ya tamasha la Singida Big Stars Day ambalo limeanza tangu asubuhi likijumuisha burudani mbalimbali.

Bao hilo pekee limefungwa na Deus Kaseke kwa shuti kali mnamo dakika ya 15 baada ya mabeki wa Zanaco kushindwa kuuondoa mpira wa krosi kutoka kwa Amissi Tambwe.

Wageni hao wa Ligi Kuu wameuanza mchezo huo kwa maelewano makubwa wakitawala dakika 15 za kwanza na kutengeneza mashambulizi kadhaa langoni mwa wapinzani wao.

Hata hivyo, Zanaco FC walirejea mchezo kadri muda ulivyosogea na kuwadhibiti wachezaji hatari wa Singida Big Stars katika safu ya mbele wakiongozwa na Amiss Tambwe, Deus Kaseke, Dario Frederico na Peterson Cruz.

Bao hilo limedumu kwa dakika zote 45 za kipindi cha kwanza ambapo Singida Big Stars imekwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa bao 1-0.

Advertisement

Nyota wawili raia wa Brazil, Dario Frederico na Peterson Cruz wameonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo wakitengeneza nafasi na kupokonya mipira huku beki wa kulia, Juma Abdul 'Mnyamani' akikumbushia makali yake ya kumimina krosi hatari (kumwaga maji).

Kikosi cha Singida Big Stars kilichoanza leo ni Benedict Haule, Juma Abdul, Shafik Batambuze, Paschal Wawa, Biemes Corno, Deus Kaseke, Said Ndemla, Peterson Cruz, Amissi Tambwe na Dario Frederico.

Kipindi cha pili cha mchezo huo unaochezwa na Mwamuzi Ahmed Arajiga kitaendelea muda mfupi ujao katika uwanja wa Liti mkoani Singida.

Advertisement