Kapombe apewa mwaka mmoja Simba

Muktasari:
- Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kuhusiana na Simba kumsainisha Kapombe, hivyo wakati wowote kuanzia sasa klabu hiyo itatangaza kuendelea naye msimu ujao wa 2024-2025.
SIMBA imemuongezea mkataba wa mwaka mmoja beki wake wa kulia, Shomari Kapombe ambao ndani yake una kipengele cha akifanya vizuri ataongezewa mwingine.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kuhusiana na Simba kumsainisha Kapombe, hivyo wakati wowote kuanzia sasa klabu hiyo itatangaza kuendelea naye msimu ujao wa 2024-2025.
"Tumemalizana na Kapombe, hivyo bado ni mchezaji halali wa Simba, tutaendelea kufaidi huduma yake na uzoefu wake kwani ni kati ya wachezaji wazawa ambao wana nidhamu ya kutunza vipaji na viwango vyao," kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba.
Kabla ya Kapombe kuongezewa mkataba huo, alikuwa anahusishwa kujiunga na Singida Black Stars na Namungo ambapo mtoa taarifa wetu amebainisha kwamba: "Ni kweli Kapombe alipata ofa mbalimbali za timu za hapa ndani na nje.
"Mashabiki wa Simba waendelee kuamini viongozi wao wanasajili wachezaji wa maana, hivyo msimu ujao utakuwa wa burudani na kufurahia mafanikio."
Kapombe amekuwa ndani ya Simba tangu Julai 2017 alipojiunga na timu hiyo akitokea Azam FC ambapo amefanikiwa kuipa mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Pia amekuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo kucheza robo fainali tano katika misimu sita ya michuano ya kimataifa tangu 2018-2019 hadi 2023-2024.
Wakati huohuo, Klabu ya Simba imethibitisha kumpa mkataba wa miaka miwili Israel Patrick Mwenda kuendelea kusalia katika kikosi cha timu hiyo hadi 2027.
Mwenda ambaye alijiunga na Simba Julai 2021 akitokea KMC, alibakiwa na mkataba wa mwaka mmoja kikosini hapo kabla ya kupewa mwingine wa miaka miwili.
Taarifa ya Simba ilisema: "Mlinzi, Israel Patrick Mwenda amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kusalia katika kikosi chetu.
"Israel ambaye anamudu kucheza kama mlinzi wa kulia na kushoto, alijiunga nasi Julai, 2021 akitokea KMC. Israel ni miongoni mwa wachezaji ambao Simba tunaamini katika uwezo wake na katika kujenga timu mpya kuelekea msimu ujao wa 2024/25.
"Israel ni mchezaji kijana ambaye bado ana nguvu ya kuitumikia timu na uwezo alionao tuna matarajio makubwa juu yake na ataendelea kusalia kwa miaka mitatu mingine."