Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanumba bado analiza watu

Muktasari:

  • Mwanaspoti lilikuwa katika eneo hilo la makaburi tangu majira ya saa tatu asubuhi na kushuhudia watu wasiozidi 30, huku wengi wao wakiwa wasanii wasio na majina makubwa.

WADAU wa tasnia ya filamu na familia ya gwiji wa zamani wa filamu Bongo, marehemu Steven Kanumba, jana waliungana kuadhimisha miaka sita tangu kufa kwake, huku wasanii kiduchu wakijitokeza katika ibada yake iliyofanyika makaburi ya Kinondoni Jijini Dar es Salam.

Mwanaspoti lilikuwa katika eneo hilo la makaburi tangu majira ya saa tatu asubuhi na kushuhudia watu wasiozidi 30, huku wengi wao wakiwa wasanii wasio na majina makubwa.

Akizungumzia uwepo wa watu wachache na kukosekana kwa baadhi ya watu wa karibu wa marehemu, mama wa Kanumba, Flora Mtegoa, alisema jambo hilo amelizoea kwani hii sio mara ya kwanza tangu alipoanza kuadhimisha siku ya mwanae kwa wasanii kujitokeza wachache.

“Huu mwitikio wa wasanii kuhudhuria kwa idadi ndogo ni kawaida yao tangu tulipomaliza kuadhimisha mwaka mmoja wa kufa kwake, lakini mimi nasema kila nafsi itaonja mauti kwani kuna wengine wanajiona wamefika na hawatakufa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mama Kanumba alikishukuru kikundi cha Sanaa cha Soweto ambacho mwaka huu kimejitolea katika kuyafanya maadhimisho hayo kwa kudai kwamba ni wachanga katika tasnia ya filamu lakini wameguswa kwa kuondokewa na Kanumba.

“Ukimuona Simba kakonda usimuite Mbwa. Hawa kwa vile ni wasanii wadogo nilidhani hawataweza walivyoniletea wazo lao la kuifanya hii shughuli ya kumbukumbu, lakini wameweza kwa kweli nashukuru kwa kazi waliyoifanya,”alisema.

Akiongelea nini anakumbuka kutoka kwa Kanumba katika miaka hiyo sita tangu alipofariki, Flora alisema ni vitu vingi na kila siku kwake anaiona kama ni jana huku akiwasema wale ambao wamekuwa wakijiuliza kwa nini kila siku analia ni kutokana na uchungu alionao kwa kumpoteza mwanae huyo wa kiume pekee kati ya watoto watatu aliojaliwa kuwapata.

“Kuna wale wanaosema mama Kanumba msiba umeisha analia nini, mimi nasema nitaendelea kulia hadi naingia kaburini, hata nikiishi miaka 800, mimi huyu nitaendelea kumlilia,”alisema mama Kanumba.

Kwa upande wake mmoja wa wasanii waliofanya kazi nyingi na Kanumba, Paster Miyamba, aliyeshiriki ibada hiyo, alisema marehemu atabaki kuwa moyoni mwake kwa kuwa ana mchango mkubwa katika sanaa yake na ndiye aliyemfanya ajulikane kwenye filamu hadi leo.

Naye Stanley Msungu, alisema wakati wakiwa kwenye kaburi la Kanumba wanafanya Ibada, alitamani ainuke na kusema kitu kwao lakini ndio hivyo haiwezekani.

Keita Nestory,mwalimu wa kikundi cha Soweto, alisema mwaka huu wameamua kuibeba shughuli hiyo kutokama na kutambua mchango wa Kanumba kama mlezi wao enzi za uhai wake.