Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kally Ongala apata pointi ya kwanza Ligi Kuu akiiongoza KMC

Muktasari:

  • Katika mchezo huo uliomalizika kwa matokeo ya 0-0, ulikuwa ni wa tatu kwa Ongala kwenye Ligi Kuu Bara tangu akabidhiwe kikosi hicho Novemba 14, 2024 akichukua nafasi ya Abdihamid Moallin aliyetimkia Yanga.

KALLY Ongala ambaye ni Kocha Mkuu wa KMC, amefanikiwa kuiongoza timu hiyo kupata pointi moja katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa uliochezwa leo Desemba 12, 2024 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliomalizika kwa matokeo ya 0-0, ulikuwa ni wa tatu kwa Ongala kwenye Ligi Kuu Bara tangu akabidhiwe kikosi hicho Novemba 14, 2024 akichukua nafasi ya Abdihamid Moallin aliyetimkia Yanga.

Mbali na kupata pointi hiyo moja leo, pia ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Ongala kukaa katika benchi kwenye mchezo wa ligi baada ya kushindwa kufanya hivyo mechi mbili zilizopita dhidi ya Dodoma Jiji na Tabora United kutokana na awali kutokuwa na vibali vya kazi.

Kabla ya leo, Ongala alikaa benchi kwenye mchezo uliopita wa Kombe la FA waliposhinda 5-0 dhidi ya Black Six.

KMC ambao walikuwa wenyeji wa mchezo wa leo, walianza vizuri lakini walikosa ubunifu zaidi eneo la mwisho kutokana na kupoteza mipira mingi kila walipofika hapo.

Mashujaa inayonolewa na Abdallah Mohamed 'Bares' nayo mara kadhaa ilijibu mapigo lakini mashambulizi yao hayakuwa na madhara.

Licha ya kwamba timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji kwa nyakati tofauti, lakini hayakufanikiwa kubadili ubao wa matokeo na hadi mwisho timu hizo kushindwa kufungana.

Matokeo hayo yameifanya KMC kutopata ushindi katika mechi nne mfululizo za ligi tangu mara ya mwisho Oktoba 31, 2024 iliposhinda 1-0 uwanja wa nyumbani dhidi ya Namungo.

Baada ya hapo, ikapoteza mechi tatu dhidi ya Simba (4-0), Dodoma Jiji (2-1) na Tabora United (0-2) kabla ya leo kupata matokeo ya 0-0 mbele ya Mashujaa.

KMC kwa sasa imefikisha pointi 15 kutokana na kucheza mechi 14 ikishika nafasi ya 11 huku ikibakiza mchezo mmoja nyumbani dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Desemba 16, 2024 kukamilisha mzunguko wa kwanza.

Kwa upande wa Mashujaa, hii ni sare ya pili mfululizo baada ya Novemba 30, 2024 ikiwa nyumbani kutoka 1-1 dhidi ya Kagera Sugar. Timu hiyo imefikisha pointi 18 katika nafasi ya sita ikicheza mechi 13.

Mashujaa imebakiza mechi mbili dhidi ya JKT Tanzania (Desemba 15) na Yanga (Desemba 19) zote ugenini ili kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Kikosi cha KMC; Wilbol Maseke, Hance Masoud/Shomary Rahim, Salum Salum, Rashid Chambo, Redemtus Mussa/Jean Nziyimana, Ismail Gambo, Pascal Mussa, Freddy Tangalo/Deogratius Kulwa, Daruesh Saliboko/Ali Shaban, Kenny Ally na Nickson Mosha.

Kikosi cha Mashujaa; Patrick Munthali, Abdulmalick Zakaria, Idrisa Stambuli, Abdulnasir Assa, Ismail Mgunda/David Ulomi, Abdulrahman Mussa/Jeremanus Josephat, Hassan Haji, Crispin Ngushi/Emmanuel Mtumbuka, Yusuf Dunia, Karlos Protas na Peter Moses.