Kaizer Chiefs yamkomalia Fei Toto
Muktasari:
- Nyota huyo wa Azam maarufu kama ‘Fei Toto’ amevutia macho ya mabosi wa Chiefs kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao na kuongoza mashambulizi.
MIAMBA ya soka ya Afrika Kusini, Kaizer Chiefs imeonyesha dhamira ya kuvunja mfumo wake wa malipo ili kumsajili kiungo wa kati wa kimataifa wa Tanzania, Feisal Salum katika dirisha dogo la usajili la Januari, mwakani.
Nyota huyo wa Azam maarufu kama ‘Fei Toto’ amevutia macho ya mabosi wa Chiefs kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao na kuongoza mashambulizi.
Feisal amekuwa kwenye kiwango bora zaidi tangu msimu uliopita alipofunga mabao 19, jambo ambalo limeifanya Chiefs kumuona kuwa mchezaji sahihi atakayeleta utofauti kwenye safu ya ushambuliaji.
Azam wanapambana kumbakiza kiungo huyo muhimu kwa kumpa mkataba mpya wenye mshahara mkubwa zaidi, lakini vita ya usajili imechukua sura mpya baada ya Simba na Chiefs kuonyesha nia kubwa ya kumnasa.
Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen huko Afrika Kusini, Chiefs wapo tayari kutumia kiasi kikubwa cha fedha ili kuhakikisha mchezaji huyo anajiunga na kikosi chao.
Hii inajumuisha ofa bora zaidi kuliko kile ambacho Azam au Simba wanaweza kutoa. Hata hivyo, kuondoka kwa Feisal Tanzania itategemea na mafanikio ya mazungumzo ya pande husika.
Chiefs wanaamini kuwa kuongeza mchezaji wa kiwango cha juu kama Feisal ni muhimu katika azma yao ya kurejea kileleni mwa soka la Afrika Kusini. Wana uwezo wa kifedha wa kuvunja mkataba wowote, lakini watakabiliana na changamoto ya kumshawishi Feisal mwenye mabao matatu na asisti nne msimu huu kuondoka nyumbani Tanzania, ambapo anapewa nafasi kubwa ya kucheza kila mara.
Hivi sasa, mishahara ya wachezaji wa Chiefs iko kwenye ngazi mbalimbali huku Zitha Kwinika akipokea R370,000 (Sh53.9 milioni), Ashley du Preez na Yusuf Maart wakipokea R300,000 (Sh 43.7 milioni) kila mmoja.
Ingawa klabu hiyo ina rekodi ya kulipa mishahara mikubwa zaidi nahodha wa zamani Itumeleng Khune anadaiwa alikuwa akilipwa R480,000 (Sh69.9 milioni) kabla ya kuondoka.
Akizungumzia dili hilo, kocha wa Chiefs, Nasreddine Nabi ambaye anadaiwa kupendekeza jina la fundi huyo aliyewahi kufanya naye kazi Jangwani, alisema: “Fei ni mchezaji wa Azam na naheshimu hilo, hivyo siwezi kusema lolote na nafurahia mwenendo wake.”
Kabla ya kujiunga na Azam, Feisal alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Yanga SC, ambapo alijijengea jina kama kiungo mwenye uwezo wa kipekee wa kuchezesha timu na kufunga mabao. Kuondoka kwake Yanga kuelekea Azam kulisababisha mvutano mkubwa, lakini sasa Chiefs wanataka kutumia nafasi hiyo kumleta Afrika Kusini.
Mashabiki wa Chiefs wanatarajia ujio wa Feisal kuwa suluhisho la matatizo yao ya kiungo mshambuliaji, nafasi ambayo imekuwa ikihitaji uimarishaji kwa muda mrefu. Uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho, kupiga mashuti ya mbali, na kufunga mabao unatabiriwa kuimarisha kikosi cha Amakhosi katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Kwa upande mwingine, Azam hawataki kumpoteza mchezaji wao muhimu na wanafanya kila jitihada kumbakiza kwa ofa mpya ya kuvutia.
Hata hivyo, Chiefs wanaamini kuwa fedha zitakuwa na nguvu kubwa zaidi ya kumbadili mawazo Feisal, ambaye anaonekana kuvutiwa na changamoto mpya.
Simba, wapinzani wa karibu wa Azam, nao wapo kwenye mbio za usajili wa Feisal, lakini Kaizer Chiefs wanaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi kutokana na nguvu ya kifedha na sifa yao kubwa barani Afrika. Hii inatoa changamoto ya kipekee kwa Azam kuhakikisha hawapotezi kiungo wao tegemezi.
Iwapo Feisal atajiunga na Kaizer Chiefs, atakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza kwa mabingwa hao wa zamani wa Afrika Kusini.
Hii itakuwa hatua kubwa kwa mchezaji huyo na soka la Tanzania kwa ujumla, huku ikiimarisha nafasi ya Tanzania kwenye ramani ya soka la kimataifa.