Kagere, Niyonzima kuibeba Rwanda kwa Cape Verde?

Muktasari:
Wakati Tanzania ikitarajiwa kucheza Ijumaa Novemba 13 dhidi ya Tunisia kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa Afcon, wawakilishi watatu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambao ni Burundi, Kenya na Rwanda watatupa karata zao leo, Jumatano.
BAADA ya kutoka majeruhi mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere leo Alhamisi Novemba 12 ataiongoza timu yake ya taifa la Rwanda kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) wakiwa ugenini dhidi ya Cape Verde.
Kagere ambaye aliukosa mchezo wa watani wa jadi kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya nyama za paja, alikuwa na ruhusa maalum kutoka kwenye benchi la ufundi la klabu yake kujiunga na timu yake ya Taifa ambayo ilianza kambi ya kujiandaa na mchezo huo.
Awali Kagere alionekana kuanza mazoezi binafsi kwa ajili ya kujiweka sawa lakini baadae akaonekana kuwa sawa na kuingia kwenye programu za mazoezi na wachezaji wenzake kwenye kikosi hicho cha Amavubi kinachonolewa na Vincent Mashami.
Kagere anatarajiwa kushirikiana na kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima ambaye naye aliukosa mchezo wa Kariakoo Derby, Jumamosi ya wiki iliyopita kutokana na kutokuwa fiti ikiwa ni siku chache tangu arejee kwenye kikosi hicho akitoka kuumwa.
Kama ilivyokuwa kwa Kagere, Haruna naye alipewa ruhusa na kocha wake, Cedrick Kaze ili awahi kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Cape Verde ambao wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi lao F linaloongozwa na Msumbiji.
Mchezaji mwingine anayechezea Bongo na ameanza kwenye kikosi hicho ni Ally Niyonzima anayekipiga Azam FC.
Rwanda wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kuweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa Fainali zijazo za Mataifa ya Afrika, wao ndio wanaburuza mkia kwenye kundi lao wakiwa na hawajapata pointi kwenye mchezo hata mmoja kati ya miwili waliyocheza.