Kagera Sugar yatema nane

Muktasari:

  • Msimu uliopita Kagera Sugar haikuwa na matokeo mazuri na kusababisha kunusurika kushuka daraja dakika za mwisho.

Kagera Sugar imewatema nyota wake nane ambao wamemaliza mikataba yao, huku uongozi ukiahidi kuboresha kikosi chake zaidi kuhakikisha msimu ujao wanafanya kweli haswa kwa kuziba nafasi hizo.

Kagera Sugar katika msimu wa Ligi Kuu iliomalizika hivi karibuni haikuwa na matokeo mazuri licha ya kufanikiwa kubaki katika michuano hiyo dakika za mwisho, huku ikifundishwa na makocha wawili tofauti.

Kwa muda mrefu timu hiyo ya mkoani Kagera ilikuwa chini ya Mecky Maxime kabla ya mambo kumuwia magumu na kujikuta akiachana nao na nafasi yake kuchukuliwa na Francis Baraza ambaye amemaliza nao msimu.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Masoud Ally amethibitisha kutowaongezea nyota nane kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi na wengine kuamua kuondoka kusaka changamoto mpya.

Aliwataja wachezaji hao ambao hawatakuwa katika kikosi chao msimu ujao kuwa ni Kipa, Benedict Tinoko, Ally Sonso, Mohamed Ibrahim, Mussa Mosi,Abdulswamad Kassim Haroun Mussa, Hassan Isihaka na Vitalis Mayanga.

"Bado ni mapema kusema wangapi tumesajili, ila tutajaza nafasi za wachezaji hao kulingana na mahitaji ya timu, kimsingi tunatarajia kuwa na kikosi bora" amesema Masoud.