Juma Abdul mguu nje, mguu ndani

BEKI wa zamani wa Yanga, Juma Abdul amesema kwa sasa anafikiria zaidi kucheza soka la kulipwa na kuna dili analisubiri na kama likitiki tu anasepa.
Beki huyo mtaalamu kwa krosi maridadi amesema kwa sasa hajasaini timu yoyote hapa nchini labda dili lake la kwenda nje likwame ndipo anaweza kufikiria timu nyingine ya kwenda.
Abdul pamoja na beki mwingine wa kati, Kelvin Yondani walitangazwa kuachwa na Yanga klabu ambayo waliitumikia kwa miaka nane.
Ilidaiwa Yanga iliachana na wachezaji hao kwa madai ya kushindwana katika maslahi.
Hata hivyo ndani ya siku mbili hizi kumeibuka maneno kuwa klabu hiyo imepanga kuwaita tena mezani wachezaji hao wazoefu ili kufanya nao mazungumzo ya kuwemo katika kikosi hicho msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Mwanaspoti Online imemtafuta Abdul leo Jumanne Agosti 25,2020 ili kuthibitisha kama ni kweli viongozi wamewaita tena mezani ambapo amejibu "Sijapata hizo taarifa zaidi ya kusikia kama wewe na sidhani kama zina ukweli”
Alipoulizwa kama ni kweli je yupo tayari kurudi Yanga, amesema, "Siwezi kujibu hilo, ni ngumu kutoa jibu la moja kwa moja wakati huu”
"Ujue kwa sasa nafikiria zaidi kwenda nje ya nchi kwa sababu kuna dili nalisubiria na kama likienda vizuri naenda kucheza huko”
"Siwezi kusema nani ananifanyia dili hilo wala timu gani inanihitaji ila ndani ya siku tatu hivi nitajua mustakabali na uelekeo wangu wa wapi nitaenda" amesema Abdul.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambao ni wadhamini wa Yanga na mjumbe wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo Hersi Said alipoulizwa kuhusu tetesi za kuwarejesha wachezaji hao, alijibu kwa ufupi "Hakuna kitu kama hicho"
Hata hivyo Abdul amesema kama dili la kwenda nje halitafanikiwa kwa sasa anaweza kusaini timu yoyote ya Ligi Kuu kwa mkataba usiozidi miezi sita.
"Hata kama hilo dili la nje halitafanikiwa kwa sasa, naweza kusaini timu yoyoye kwa miezi sita tu wakati naendelea kufanya mipango mingine ya kucheza nje ya nchi"amesema Abdul.
Moja ya timu inayomuhitaji mchezaji huyo hapa nchini ni Namungo ambayo itashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.