Mlandege yaizima Mwembe Makumbi Ligi Kuu Zanzibar

Muktasari:
- Dakika 90 za mchezo wa wababe wa ligi hiyo M/Makumbi na Mlandege imemalizika kwa ushindi wa bao 2-0 kwenye Uwanja wa Mao A, Mjini Unguja.
VINARA wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Mwembe Makumbi imekumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mlandege katika pambano kali lililopigwa kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja.
Katika pambano la duru la kwanza timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kufungana mabao 2-2 kwenye Uwanja wa New Amaan na leo ikiwa moja ya mechi za raundi ya 23 Mlandege ikafanya kweli kwa ushindi huo.
Katika mechi ya leo, Mlandege iliandika bao la kwanza dakika ya 11 kupitia kwa Abdallah Idd lililodumu hadi mapumziko.
Bao la pili la Mlandege lilifungwa dakika ya 50 likiwekwa pia na Abdallah Idd na kuifanya timu hiyo ifikishe pointi 44, moja pungufu na ilizonazo Mwembe Makumbi inayoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na 45 kila moja ikicheza mechi 23.
Katika mchezo mwingine uliopigwa kisiwani Pemba kwenye Uwanja wa Finya, Chipukizi na Mwenge zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu.
Ligi hiyo itaendelea kesho Jumapili kwa Malindi kuumana na KMKM kwenye Uwanja wa Mao A, ilihi Kipanga itacheza na Mafunzo.