Jogoo: Heshima yetu RBA itarudi tu

Muktasari:
Timu hiyo inajifua kila siku saa 11 Jioni hadi saa 3 Usiku kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Zanaki ambapo kwa mujibu wa kocha wao, lengo ni kuhakikisha wanarudisha heshima ya Jogoo kwenye mpira wa kikapu.
LICHA ya kusuasua kwa timu ya mpira wa kikapu ya Jogoo kwenye Ligi ya mkoa wa Dar es Salaam (RBA), kocha mkuu wa timu hiyo, Ashraf Haruni amesema Jogoo haiwezi kushuka daraja na siku si nyingi watarudisha heshima ya timu hiyo kwenye kikapu.
Timu hiyo imecheza mechi 12 na kufungwa zote kwenye RBA inayoelekea ukingoni katika mzunguko wa kwanza.
Jogoo yenye Pointi 12 inaning’inia kwenye msimamo ikiwa ndiyo timu iliyofungwa mechi nyingi ikifuatiwa na Segerea BC ambayo pia haijaonja ladha ya ushindi katika michezo yake 11 iliyocheza.
“Tatizo kikosi chetu cha awali kilibadirika, wachezaji tuliokuwa nao walikwenda kwenye majukumu mengine tukaanza upya,” alisema kocha wa Jogoo, Ashraf Haruni.
Alisema licha ya kusuasua kwenye mzunguko wa kwanza, lakini atapambana kuhakikisha timu hiyo haishuki daraja.
“Vijana wameanza kuzoea Ligi, mechi ya mwisho tuliyocheza pamoja na kupoteza, lakini tulicheza vizuri, hii ni dalili njema kwetu,” alisema kocha huyo.
Alisema baada ya mzunguko wa kwanza anaamini watarudi tofauti kwenye mzunguko wa pili na mechi 15 za mzunguko huo zitawabakisha kwenye RBA.
Timu hiyo inajifua kila siku saa 11 Jioni hadi saa 3 Usiku kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Zanaki ambapo kwa mujibu wa kocha wao, lengo ni kuhakikisha wanarudisha heshima ya Jogoo kwenye mpira wa kikapu.
Mbali na Jogoo, timu nyingine iliyopanda daraja ya Segerea BC imeanza vibaya Ligi hiyo kwa kufungwa mechi zote 11 ilizokwishacheza mpaka sasa ikiwa inakamata mkia kwenye msimamo na pointi 11 kitu ambacho kinaonekana kuzidi kuwatisha vijana hao kwenye RBA.