Prime
Job amaliza utata Yanga

Muktasari:
- Katika hilo, kuna nyota kadhaa wanaomaliza mikataba mwishoni mwa msimu huu akiwemo beki na nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Dickson Job.
KIPINDI hiki cha kuelekea kumalizika kwa msimu, taarifa ambazo Wanayanga wanahitaji kuzisikia mbali na mambo mengine, ni maendeleo ya kikosi chao na mustakabali wa mastaa wa kikosi hicho hasa wale mikataba yao inayoelekea ukingoni.
Katika hilo, kuna nyota kadhaa wanaomaliza mikataba mwishoni mwa msimu huu akiwemo beki na nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Dickson Job.
Taarifa mpya kutoka Yanga zinabainisha kwamba, beki huyo amemaliza utata klabuni hapo baada ya kuongeza mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo.
Job alisaini mkataba huo Jumamosi iliyopita baada ya kufikia makubaliano ya nyongeza ya mshahara na dau la usajili na kuzima tetesi kwamba alikuwa mbioni kuibukia klabu nyingine kutokana na ofa zilizokuwa mezani kwa menejimenti ya beki hiyo wa kati anayeitumikia pia timu ya taifa, Taifa Stars.
Mkataba wa awali wa beki huyo mwenye umri wa miaka 24 na Yanga ulikuwa ufikie tamati baada ya msimu huu kumalizika, lakini mahitaji ya timu hiyo kuendelea naye, yamemfanya nyota huyo aliyezitumikia timu zote za taifa za kiume kuanzia ile ya umri wa miaka 17 hadi ya wakubwa kubakia.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga kimethibitisha kuwa beki huyo ameshamalizana na klabu hiyo na kilichobaki ni utambulisho tu wa mkataba huo mpya.
“Tulishafunga hesabu za Job (Dickson) tangu Jumamosi iliyopita na tunasubiria tu kutangaza jukumu ambalo limeachwa kwa idara ya habari ambayo yenyewe ndio itaandaa siku na namna ya kutoa taarifa,” kimefichua chanzo hicho.
Hata hivyo, meneja wa mchezaji huyo, George Job alipotafuta kufafanua juu ya dili hilo, alisema kuwa bado beki huyu hajasaini mkataba mpya, lakini wapo mbioni kukamilisha suala hilo.
“Bado tupo kwenye mazungumzo, lakini bado Dick hajasaini,” alisema Job.
Tangu alipojiunga na Yanga Januari 2021 akitokea Mtibwa Sugar, Dickson Job amekuwa mchezaji tegemeo wa Yanga kutokana na kiwango bora alichokionyesha ndani ya timu hiyo.
Mchezaji huyo katika msimu wa 2022/2023 aliibuka mshindi wa tuzo ya beki bora wa msimu huku akiingia katika kikosi bora cha msimu mara tatu mfululizo.
Katika msimu huu, mchezaji huyo amecheza idadi ya mechi 24 za Yanga katika Ligi Kuu kwa dakika 2,094, akiwa ameunda pacha tegemeo ya ulinzi ya kikosi cha timu hiyo sambamba na beki Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ ambayo pia ndio imekuwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Dickson Job ndiye amewahi kuwa nahodha wa timu za taifa za vijana za Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’.