JIWE LA SIKU: Sababu vifo vya ghafla kwa wachezaji uwanjani

IDADI ya vifo kwa wachezaji kufia uwanjani inazidi kuongezeka nchini huku wadau na wataalamu wa afya wakielezea sababu na namna ya kuepukana na matukio hayo ili kulinda afya zao.

Kwa miaka 10 ya karibuni wachezaji takribani tisa walidondoka uwanjani na kupoteza maisha wakiwa katika majukumu yao, hali ambayo inatia hofu na wasiwasi kwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Katika mwaka 2015, aliyekuwa mchezaji wa timu ya vijana ya Coastal Union, Mshauri Salim alipoteza maisha alipoanguka uwanjani wakati wa mazoezi na kupoteza maisha.

Mwaka 2016, aliyekuwa straika wa timu ya vijana (U20) ya Mbao FC, Ismail Khalfan alianguka na kufariki dunia wakati timu yake ikicheza dhidi ya Mwadui kwenye ligi ya vijana ya TFF kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kama haitoshi, mwaka 2022 mchezaji wa Singida FG, Mohamed Banda alianguka akiwa uwanjani wakati wa mazoezi ya timu hiyo mjini Singida na kupoteza maisha.

Mwaka jana jinamizi liliendelea huko mkoani Songwe, ambapo mchezaji Albert Andrea aliyekuwa akiichezea Saza FC aligongana na mwenzake uwanjani na kufariki dunia.

Machozi yalizidi kuwatiririka wadau na mashabiki wa soka nchini kwa aliyekuwa beki wa Mtibwa Sugar, Iddy Mobby kufariki dunia akipatiwa matibabu hospitalini Dodoma baada ya kuumwa ghafla wakati wa mazoezi binafsi.

Pia simanzi imeendelea kutawala mwaka huu (2024), ambapo mchezaji Bille Mgala alipoteza maisha wakati timu yake Manchester FC ikijipima nguvu dhidi ya Super Eagle katika mchezo wa kirafiki huko Mbozi Songwe.

Hata hivyo, sio matukio hayo tu kwani mwaka 1979 aliyekuwa mchezaji wa Simba, Husein Tindwa alindondoka uwanjani na kufariki dunia kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Racca Rovers ya Nigeria.

Pia lipo tukio la kifo cha aliyekuwa mchezaji wa AFC ya jijini Arusha, Nadhir Mchomba aliyefariki uwanjani mwaka 2001 wakati wa mechi dhidi ya 44KJ ya jijini Mbeya.

Mbali na vifo vya wachezaji, hata mashabiki nao hukumbana na matukio hayo haswa wanapokuwa wakishangilia timu zao, na pia wananchi wa kawaida nao hujikuta kwenye changamoto hizo.


WASIKIE MADAKTARI

Daktari wa Geita Gold, Abdalah Chuma anasema vipimo vya mara kwa mara kwa mchezaji ni muhimu sana katika kubaini afya yake ili kusaidia ufanisi wake kwenye kazi.

Anasema matukio ya wachezaji kudondoka uwanjani na kupoteza maisha yanafikirisha sana na inahitaji huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa kituo cha afya au hospitalini.

Anasema mchezaji anaweza kuwa na matatizo yoyote ya kiafya ikiwamo mapigo ya moyo, kisukari na mengineyo hivyo anapokuwa uwanjani bila kujua changamoto yake madhara humtokea.

Pia anataja matumizi ya dawa za kienyeji, vidonge na unywaji wa energy drinks vinaweza kusababisha changamoto za kiafya kwa mchezaji akieleza kuwa timu nyingine haswa za madaraja ya chini hazina wataalamu.

“Mchezaji anapodondoka zipo hatua za kufuata, ikiwamo kuwahi ulimi wake umekaaje, kumpiga mashavu kama atajibu chochote, au kumuita akajieleza kubaini kama amejitambua,” anasema na kuongeza:

“Mchezaji kama ameanguka na kupata tatizo kubwa hapaswi kupewa chochote cha kula au kinywaji, unaweza kumpiga maeneo tofauti ili kuona atajibu au kuwa kimya,” anasema Dk Chuma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Tiba katika Hospitali ya Mbozi Mission mkoani Songwe, Dk Julius Mnkondya anasema tatizo kubwa la wachezaji haswa wa timu za chini hawapimi afya zao.

Anasema mbali na wachezaji hata watu wengine wakiwamo mashabiki wanapaswa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ili kubaini tatizo kabla ya kukutwa na changamoto yoyote.

“Kama yule mchezaji (Bella) aliyefariki juzi hapa Songwe alipodondoka ilibainika kuangukia kisogo na ubongo kutingishika, hadi anafikishwa hapa hospitalini alikuwa ameshakata roho.

“Hatuwezi kujua alikuwa akisumbuliwa na tatizo jingine au la, lakini hata mashabiki wenyewe wanapaswa kuwa na tahadhari ya kupima afya ili kujiepusha na matukio ya presha,” anasema Dk Julius.

Mganga mkuu msaidizi huyo katika hospitali hiyo, alizitaka timu zote haswa za madaraja ya chini kuwa na wataalamu wa afya wenye ujuzi ili inapotokea tukio la wachezaji kuanguka uwanjani wapatiwe huduma ya kwanza.

“Kuna mmoja wa mashabiki hapa Songwe wakati wa mechi ya Yanga na Azam alipoona Azam anashambulia sana alianguka hadi leo ni kama kaparalaizi,” anasema daktari huyo.

Dokta wa Mwanaspoti, Dk Shita Samuel anasema shambulizi la moyo ‘heart attack’ ni moja ya matatizo ya kiafya yasiyoambukiza yanayosababisha mara kwa mara vifo vya ghafla kwa watu wazima.

Anasema mbali na matatizo ya moyo, katika sehemu nyingine za mwili kama figo na ubongo vinaweza kupata tatizo na kusababisha vifo vya ghafla.

“Moyo ndio ogani kubwa inayohusika na usukumaji damu mwilini, matatizo yake huwa ni kimyakimya na ndio yanaongoza kuleta vifo vya ghafla duniani,” anasema.

“Vilevile uwapo wa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo, upungufu wa madini kama magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, wingi wa mafuta mabaya mwilini na kadhalika vinachangia vifo vya ghafla pia,” anasema Dk huyo.

Anashauri kuwa kuwapo kwa elimu ya huduma ya kwanza kuanzia shuleni ili kuwajengea uwezo katika utoaji huduma hiyo kwa mtu aliyepatwa na mshutuko au shambulizi la moyo.


MDAU KAONGEA

Mwenyekiti wa chama cha soka mkoani Songwe (Sorefa), Jacob Mwangosi anasema licha ya wachezaji wengi wa timu za chini kutopima afya zao, lakini hata mazingira wanayoishi si salama sana.

Anasema timu nyingi za ngazi za chini uchumi ni mbaya kuweza kujiendesha na kuwa na wataalamu katika maeneo yote, lakini hata miundombinu ya viwanja nayo si rafiki.


WACHEZAJI HAWA HAPA

Beki wa zamani wa Mwadui, Gwambina na Coastal Union, Revocatus Mgunga anasema mechi za ndondo licha ya athari zake, lakini zinasaidia kuwaingizia kipato haswa mchezaji anapokosa timu.

Anaeleza kuwa muda mwingine viongozi wa timu wanapochelewesha malipo humfanya mchezaji kutafuta zilipo ndondo ili kuweza kutafuta riziki bila kujali afya.

“Utaishije na maisha yenyewe haya, muda mwingine mchezaji anakosa timu msimu mzima hivyo ili kutokuwa ombaomba mtaani unaamua kucheza ndondo kutafuta pesa familia ile.”

Hata hivyo, anakiri kuwa mazingira ya mechi za ndondo huwa na hatari nyingi kwani hakuna wataalamu wa afya ambapo mchezaji huzingatia tu kuingia uwanjani kucheza ili kuipa ushindi timu.

Kwa upande wa nyota wa zamani wa Majimaji, Tukuyu na Boma FC, Emmanuel Mwagamwaga anasema ndondo ni chanzo kikubwa cha matatizo ya afya kwani mechi zake huwa hazina mpangilio.