Jeuri ya Yanga ipo hapa

KIKOSI cha Yanga kinajiandaa kuondoka jijini Dar es Salaam leo Ijumaa, kwenda Tanga kwa ajili ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), ikiendelea kuupigia hesabu ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi 73 baada ya mechi 27, lakini ikifichua siri inayoibeba timu hiyo.
Yanga inayoshikilia taji la Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo, inachuana na Simba iliyopo nafasi ya pili zikitofautiana pointi nne, Simba ikiwa na 69 baada ya mechi 26, moja zaidi na ilizocheza Yanga, ambayo imeshinda 24, ikitoka sare mmoja na kupoteza miwili tu hadi sasa.
Jeuri inayoibeba Yanga ni mgawanyiko wa mabao wa nyota wa kikosi hicho ambacho kwa sasa kimefunga 71, ni sawa na idadi ya msimu uliopita na hivyo inahitaji bao moja tu kuvunja rekodi hiyo kwa klabu hiyo iliyoruhusu kufungwa mabao 10.
Katika mabao ya Yanga msimu huu kumekuwa na mwenendo mzuri kuanzia kiungo hadi washambuliaji jambo linaloonyesha wazi kwa sasa imekuwa na mabadiliko makubwa, ndiyo maana kimekuwa tishio katika kufumania nyavu za wapinzani.
Nyota wa Yanga wanaoongoza kwa mabao ni Clement Mzize na Prince Dube wenye 13 kila mmoja hadi sasa na wanawania kiatu cha ufungaji bora na msimu uliopita Mzize alifunga sita tu, rekodi ambayo tayari ameivunja huku zikiwa bado mechi tatu zimebakia.
Dube ukiwa ni msimu wake wa kwanza na timu hiyo tangu ajiunge nayo akitokea Azam FC, msimu uliopita akiwa na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam alikifungia mabao saba tu.
Dube amekuwa na msimu bora akiwa na Yanga hadi sasa na ndiye nyota aliyechangia mabao mengi ya timu hiyo Ligi Kuu akihusika na 21 akifunga 13 na kuasisti manane kati ya 71.
Stephane Aziz KI aliyeibuka mfungaji bora msimu uliopita Ligi Kuu Bara akiwa na timu hiyo baada ya kufunga mabao 21, msimu huu amepunguziwa majukumu zaidi ya ufungaji kutokana na uwepo wa washambuliaji, Dube na Mzize.
Msimu huu, Aziz KI amefunga mabao tisa, sawa na kiungo mwenzake, Pacome Zouzoua na ni idadi kubwa kwake, kwani msimu uliopita nyota huyo alimaliza na mabao saba, japo angeweza kufunga pia zaidi kama isingekuwa majeraha ya mara kwa mara. Maxi Mpia Nzengeli aliyefunga mabao 11 msimu uliopita, tayari msimu huu amefunga matano na kuasisti tisa, akizidiwa tu na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC anayeongoza msimu huu, akiasisti 13 hadi sasa.
Msimu uliopita, mbali na Aziz KI na Maxi waliofunga mabao mengi zaidi ya kikosi cha Yanga, ila wengine ni Mudathir Yahya aliyefunga tisa, ingawa hadi sasa msimu huu, kiungo huyo amefunga mawili na kuasisti matatu.
Kwa upande wa mabeki, nako kumekuwa na vita ya aina yake na hadi sasa Yanga anayeongoza ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’ mwenye mabao manne, huku Israel Mwenda akifunga mawili, ikiwa ni mgawanyiko mzuri kwenye kila maeneo.
Ushindi wa mabao 3-0, ilioupata Yanga dhidi ya Namungo, Mei 13, 2025, umeifanya pia timu hiyo kufikisha mechi 17 za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza, tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 3-1 na Tabora United, Novemba 7, 2024.
Katika mechi 17, Yanga imeshinda 16 na kutoka suluhu moja tu, ikizidiwa mitatu na wapinzani wao, Simba iliyofikisha 20, bila kupoteza, ikishinda 18 na kutoka sare miwili, tangu ilipochapwa katika ‘Dabi ya Kariakoo’ bao 1-0, Oktoba 19, 2024.
Mbali na hilo, ila Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi amekuwa na mwenendo mzuri katika kikosi hicho kwani hadi sasa hajapoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu aliyoiongoza (10) na ameshinda tisa na kutoka sare mmoja tu.
Hamdi aliyejiunga na timu hiyo rasmi Februari 4, 2025, akitokea Singida Black Stars ili kuchukua nafasi ya Mjerumani Sead Ramovic, mechi yake ya kwanza ilikuwa ni ya suluhu (0-0), dhidi ya maafande wa JKT Tanzania, Februari 10, 2025.
Tangu apate suluhu hiyo, wapinzani wamekuwa na wakati mgumu wa kujibu maswali anayowapa hadi sasa, kwani ameshinda tisa kati ya 10 iliyoiongoza Yanga, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 29 na kuruhusu matatu tu.