Jabir afunguka baada ya kutua Ubelgiji

Baada ya kutua katika klabu ya KAA Gent ya nchini Ubelgiji kwa majaribio ,Anuary Jabir amesema atapambana kufanikisha ndoto yake ya muda mrefu ya kucheza soka la kulipwa.
Jabir ambaye anaichezea Kagera Sugar aliondoka juzi nchini kwenda Ubelgiji kwa ajili ya kufanya majaribio katika klabu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti kutokea nchini Ubelgiji, Jabir alisema amefurahi kupata nafasi hiyo na atapambana kuhakikisha ndoto yake hiyo inatimia.
Mshambuliaji huyo huyo ambaye amewahi kuwa mfungaji bora wa ligi daraja la kwanza msimu wa 2019-2020 wakati huo akichezea Dodoma Jiji alisema amepokelewa vizuri na wenyeji wake na anaamini atafanya vizuri katika majaribio hayo.
Straika huyo mpaka anaondoka nchini alikuwa ameifungia Kagera Sugar mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara na amewahi kuwa mchezaji bora wa ligi kuu kwa mwezi Februari mwaka 2021.