Ishu ya Mukoko iko hivi

BAADA ya kiungo Mukoko Tonombe kuchomolea mpango wa uongozi wa Yanga wa kumpeleka kwa mkopo TP Mazembe ikiwa ni sehemu ya mabadilishano na winga, Chico Ushindi na kisha bosi wa GSM, Ghalib Said, kuingilia kati na kuzuia dili hilo, uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani umefunguka kila kitu.
Kaimu mtendaji mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha Mazingisa amesema mchezaji huyo ataendelea kusalia kikosini sababu bado ana mkataba.
Senzo alisema viongozi wanajua namna ya kuendesha timu na wana mipango yao ya kutoa taarifa na kwenye suala la Mukoko bado ni mchezaji wao halali.
“Mukoko ni mchezaji wetu inategemea na mipango na mabadiliko yaliyopo, klabu itatoa taarifa rasmi kwa mashabiki wake juu ya nini kinachoendelea,” alisema Senzo.
Mukoko mwenyewe alisema wakati huu anaendelea na mazoezi ya gym, ili kuweka mwili wake sawa baada ya kukubaliana na GSM kuwa anarejea katika kikosi kama ilivyokuwa hapo awali.
“Ule mpango wa kwenda TP Mazembe tumekubaliana na bosi GSM kuwa haupo tena,” alisema Mukoko ambaye ni mchezaji bora wa kikosi cha Yanga msimu uliopita.
Katika hatua nyingine Senzo alisema ujio wa kocha mpya wa makipa, Mbrazil Milton Nienov maana yake wanakwenda kutanua benchi la ufundi ili kuwa na watu wengi wenye uelewa mkubwa wa masuala ya kiufundi.
Senzo alisema kuhusu kocha wao wa makipa aliyepo kikosini sasa hivi, Mkenya Razack Siwa ataendelea kusalia katika timu hiyo na watafanya kazi kwa kushirikiana na mwenzake.
“Razack ataendelea kuwa sehemu ya benchi la ufundi akiendelea na kazi yake, kuongezeka kwa Milton ni kwenye kujenga na kuongeza nguvu katika eneo la makipa,” alisema Senzo.
Hata hivyo, taarifa nyingine za chinichini zinadaiwa Siwa anaweza kuondoka pindi Milton akishazoea mazingira kwenye timu hiyo, ingawa wenyewe Yanga bado hawajaweka wazi jambo hili.
Yanga itaivaa Polisi Tanzania Jumapili hii mjini Moshi.