Imepania si mchezo

Muktasari:
Unajua kwa nini? Ikiwa visiwani hapa Simba inafanya yake huku makocha wakitoa mazoezi kwa ustadi wa juu, wakitengeneza kombinesheni babu kubwa. Makocha hao pia wanatoa mazoezi ya kuimarisha beki, viungo na washambuliaji, pia wanataka Simba iwe na uwezo wa kupata mabao dakika zote inapokuwa inacheza.
BAADA ya kuchoshwa na kejeli zinazotolewa na watani wao wa jadi (Yanga) wanaowaita Wazee wa Mchangani, sasa Simba imezinduka. Imeamua kuweka kila kitu kando na kufanya jambo litakaloweza kuwapa heshima msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. Kwa kifupi wamepania kweli kweli.Hivi karibuni ilienda kujificha Lushoto, Tanga kwa wiki mbili na sasa ipo chimbo la visiwani Zanzibar ikiendelea kujifua kujiandaa na msimu huo mpya utakaoanza Septemba 12.
Unajua kwa nini? Ikiwa visiwani hapa Simba inafanya yake huku makocha wakitoa mazoezi kwa ustadi wa juu, wakitengeneza kombinesheni babu kubwa. Makocha hao pia wanatoa mazoezi ya kuimarisha beki, viungo na washambuliaji, pia wanataka Simba iwe na uwezo wa kupata mabao dakika zote inapokuwa inacheza.
Kutengeneza nafasi
Kocha Mwingereza, Dylan Kerr, amekuwa akitoa mazoezi ya tofauti na amepanga kuhakikisha kwenye nafasi 45 ambazo timu yake inapata inapokuwa inashambulia basi ni lazima ifunge mabao matano au sita.
Alisema: “Tunajaribu kuiweka timu icheze kwa pamoja na itakapokuwa ikishambulia iwe inapanda na ikirudi kukaba iwe hivyo pia, hivyo tutaweza kujijengea mazingira mazuri ya kupata mabao mengi kipindi ambacho tunatengeneza nafasi.
Kombinesheni
Kocha huyo akishirikiana na wasaidizi wake, amekuwa akitoa programu maalumu yenye lengo la kutengeneza mawasiliano miongoni mwa wachezaji wa idara moja.
Kocha huyo alikuwa akizijaribu idara mbalimbali na kwa nyakati tofauti aliwachukua mabeki na kuwapambanisha na mastraika.
Pia akachukua viungo na kuwapambanisha na mastraika huku akiwataka mastraika wapambane kuhakikisha wanafunga goli huku mabeki au viungo wakihakikisha wanaharibu mipango ya washambuliaji.
“Lengo lilikuwa kutengeneza mawasiliano kati ya wachezaji wa idara fulani wanapokuwa wakicheza,” alifafanua.
“Mfano, nimeipima idara ya kiungo kwa kuwaweka Mkude (Jonas), Ndemla (Said), Banda (Abdi) na Awadh Juma na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuisimamisha timu pinzani isicheze au kwenda kokote. Hapo nilitaka kuona ni jinsi gani wanaelewana.
Mfano mwingine ni wa mastraika, nimewajaribu Mgosi (Mussa), Maguli (Elias) na Ajibu (Ibrahim).
Kombinesheni nyingine ni ya Kiiza (Hamis), Sserunkuma (Simon) na Ndemla.
Kukaba, kushambulia
Kocha huyo pia alikuwa akitoa mazoezi kwa wachezaji wote akiwataka wote wakabe pindi wanaposhambuliwa na watengeneze nafasi wanapokuwa na mpira.
Alisema: “Hauwezi kufunga kama hautengenezi nafasi, pia huwezi kushinda kama hukabi hivyo ni rai kwa kila mchezaji kukaba na kushambulia na hilo ndilo ninalowafundisha.”
Vita tupu
Idara zote zina ushindani wa kawaida, lakini tofauti iliyopo ni kwenye safu ya ushambuliaji ambayo ina washambuliaji wa kati wanne; Mgosi, Kiiza, Maguli na Ajibu. Unajua nini kinatokea?
Hapa kuna vita kubwa kati ya Ajibu na Kiiza na wamekuwa kama vile wanashindana kufunga mabao kwenye mazoezi.
Kuhusu hiko, kocha huyo anasema: “Ninahitaji wafunge, ninahitaji ushindi wa timu, kazi yao kubwa ni kufunga mabao, hivyo sitaki waniangushe.”
Kiungo na mabeki
Kocha Msaidizi, Selemani Matola, amekuwa na maelekezo mengi kwa viungo na ameeleza kuwa kwa uimara wa wachezaji kila nafasi ina wachezaji wawili wa uhakika na kila kiungo ameimarika.
Hasira za mashabiki
Kocha Kerr amekuwa akiwafuata mashibiki wanaotokea kushuhudia mazoezi na ameonekana mara kwa mara akiwaonyesha na kuwauliza kama kuna kipya kizuri.
Hata hivyo, kocha huyo anasema: “Ninajua mashabiki wa Simba wana hasira na timu yao kukosa mafanikio miaka ya hivi karibuni. Hivyo ninawaomba mtulie kipindi hiki ili niwafanye wachezaji wawe na hasira zaidi ya ushindi kuliko mashabiki.
Makocha, wachezaji Zanzibar
Katika kuhakikisha anasaidia kuinua soka la vijana Zanzibar, Kocha Kerr alikuwa moja ya vivutio vikubwa wikiendi hii baada ya kuendesha programu maalumu kwa ajili ya wachezaji mbalimbali 50 wa timu za vijana chini ya miaka 15 huku akiwahusisha kwa karibu makocha wa timu hizo.
Kocha huyo alisema: “Siwezi kuwa mchoyo wa kufundisha kile nilichonacho, ninatamani wote wapate mafanikio kisoka. Ni kazi yangu pia.”