Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huyu Kagere... Azam wamemshindwa

HAWAMUWEZI! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere kuwafunga Azam FC kwenye mechi nne za Ligi Kuu walizokutana uwanjani.

Baada ya bao alilolifunga kwenye mchezo uliopigwa juzi, Jumapili kati ya Simba na Azam uliomalizika kwa sare ya 2-2, Kagere anakuwa amefikisha mabao matano akiwafunga wanalambalamba hao kutoka Chamazi.

Tangu staa huyo wa timu ya taifa ya Rwanda asajiliwe na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya msimu wa 2018-19, Azam imeshindwa kumzuia kwenye mechi za Ligi Kuu Bara kwani ameifunga katika mechi nne timu hizo zilipokutana ndani ya misimu mitatu.

Mwanaspoti kupitia makala hii linakuletea uchambuzi wa mabao matano ya Kagere aliyoifunga Azam katika michezo minne ya ligi.


AZAM 1-3 SIMBA (2018-19)

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Kagere kukutana na Azam, pia mechi ya kwanza kuzikutanishatimu hizo mbio za Dar es Salaam kwenye ligi msimu huo.

Mchezo huo uliokuwa wa kiporo kwa Simba kutokana na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ulipigwa Februari 22, 2019 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Benjamin Mkapa), ambapo Azam walikuwa wenyeji na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Katika mechi hiyo Kagere alifunga mabao mawili - bao la kwanza aliloweka kambani dakika ya nne kwa kichwa baada ya shuti la John Bocco kugonga mwamba na mpira kumkuta kwenye eneo sahihi na kuuzamisha wavuni.

Bao la pili lilifungwa na Bocco kwa kichwa dakika ya 38 akipokea krosi safi toka kwa Zana Coulibaly aliyepiga kutokea upande wa kulia wa uwanja.

Dakika ya 77, Kagere aliifungia bao la tatu Simba na la pili kwake kwenye mechi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Chama akipiga shuti la kwanza likamgonga mlinzi Bruce Kangwa na kumalizia kwa shuti jingine liliotinga golini. Katika mchezo huo bao pekee la Azam lilifungwa na Frank Domayo dakika ya 81.


SIMBA 1-0 AZAM (2019-20)

Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa timu hizo mbili kukutana msimu wa 2019-20 ambayo ilimalizika kwa Wekundu wa Msimbazi kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo ambao wao ndio walikuwa wenyeji kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Mchezo huu ulipigwa Oktoba 23, 2019 na bao hilo pekee na la ushindi kwa Simba - Kagere alilifunga dakika ya 48 akipokea pasi kutoka kwa Francis Kahata ambaye pia ulikuwa mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baada ya kujiunga na Simba msimu huo akitoke Gor Mahia ya Kenya.


AZAM 2-3 SIMBA (2019-20)

Mchezo huo ulikuwa wa marudiano kwa msimu wa 2019-20 baada ya ule wa duru la kwanza kumalizika kwa Simba kushinda 1-0. Katika mchezo huo uliopigwa Machi 4, mwaka jana, Azam ndio walitangulia kupata bao dakika ya nne kupitia kwa Never Tigere aliyefunga kwa shuti akiwa ndani ya eneo la hatari kwa Simba akipokea pasi ya Idd Selemani. Simba walisawazisha dakika ya nane kupitia kwa Erasto Nyoni aliyefunga kwa kichwa baada ya kupokea pasi ya Clatous Chama. Dakika ya 15 ya mchezo huo Deo Kanda aliwafungia Simba bao la pili kwa kupasia nyavu baada ya kupokea pasi kutoka kwa Chama.

Azam, dakika ya 49 walisawazisha kupitia kwa Seleman ambaye alifunga akiwa katikati ya mabeki wa Simba baada ya kupigiwa pasi mpenyezo na Shaban Chilunda.

Dakika ya 71 Kagere aliifungia bao la tatu na la ushindi Simba na la nne kwake dhidi ya Azam kwa kuunganisha mpira moja kwa moja baada ya kupokea pasi ya Shomari Kapombe.

SIMBA 2-2 AZAM (2020-2021)

Ikiwa ni mechi ya kiporo kwa Simba na ya kwanza kwa timu hizo mbili kukutana kwenye ligi msimu huu ilipigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Simba ndio walikuwa wenyeji.

Katika mechi hiyo Kagere ndiye alifungua ukurasa wa mabao kwa kufunga la kwanza dakika ya 27 akimalizia krosi iliyopigwa na Luis Miquissone na kuwafanya Simba kuongoza mpaka mapumziko.

Kipindi cha pili Azam walirejea na moto na dakika ya 67 kupitia kwa Seleman walisawazisha akipiga shuti kali nje ya boksi la 18 la Simba mpira uliomshinda kipa Aishi Manula na kuzama wavuni.

Dakika ya 76 Azam walipata bao la pili kupitia kwa Ayoub Lyanga aliyefunga akiwa katikati ya mabeki wawili wa Simba akipasia nyavu baada ya kupokea pasi safi toka kwa Seleman bao ambalo halikudumu kwani Simba kupitia kwa Miquissone dakika ya 77 walipata bao la kusawazisha.

Mabao hayo matano yanamfanya Kagere kuwa mchezaji aliyewafunga mengi Azam FC ndani ya misimu mitatu ya hivi karibuni.