Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tulieni nyie bado tano!

MASHABIKI wa Yanga jana walioondoka Uwanja wa Benjamin Mkapa wakisonya baada ya Luis Misquissone kufunga bao la kusawazisha wakati Simba ikitoka sare ya 2-2 dhidi ya Azam katika mechi ya kiporo, huku mashabiki wa Msimbazi wakishangilia kwa kuimba bao tano...bado tano!

Yanga walikuwa wakiombea Simba ipoteze mchezo huo ulioshuhudia Clatous Chama kikosa penalti kipindi cha kwanza, ili kuongeza pengo la pointi baina yao, lakini bao la shuti la mwana ukome la Luis liliwakata stimu na kuwapa furaha wale wa Simba waliokuwa wamenywea.

Simba ilipata penalti hiyo baada ya Luis kuangushwa ndani ya lango la Azam na mwamuzi Martin Saanya kuamuru penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Mathias Kigonya kabla ya mpira kumrudia Chama ambaye alishindwa kuukwamisha wavuni na kuokolewa na mabeki wa Azam.

Katika mchezo huo uliokuwa mtamu na wenye ushindani mkubwa, ulikuwa ni kama wa nyota wawili wa timu hizo, Luis na Idd Seleman ‘Nado’ kwani wote walihusika na mabao ya timu zao, huku kipa Kigonya akiwa nyota wa mchezo kwa kuiokoa Azam isipoteze mchezo kwa Simba.

Nado na Luis kila mmoja aliasisti na kufunga bao moja moja kwenye mchezo huo uliochezeshwa na Saanya, huku straika Meddie Kagere akiendelea kung’ara chini ya Kocha Didier Gomes wa Simba kwa kufunga bao lake la tisa msimu huu akimpiku nahodha wake, John Bocco.

Kagere alifunga bao lake la tano dhidi ya Azam katika Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu tangu ajiunge na Simba kutoka Gor Mahia ya Kenya, kwani aliitungua mabao mawili kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya timu hiyo msimu wa 2018-2019 katika ushindi wa mabao 3-1.

Msimu uliopita alifunga mabao mawili, moja kwenye mchezo wa kwanza ambao Simba ilishinda 1-0 kisha kufunga la ushindi kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Machi mwaka huu na Simba kushinda 3-2 kabla ya jana kufunga bao la kuongoza dakika ya 27 akimalizia pasi ya Luis.

Bao hilo lilidumu hadi wakati wa mapumziko kabla ya kipindi cha pili kuanza kwa Azam kucharuka na kusawazisha bao kwa juhudi binafsi za Nado alipomtungua Aishi Manula kwa shuti la nje ya 18 dakika ya 67 kwa kumalizia pasi murua na Prince Dube aliyekuwa akirejea tena uwanjani tangu alipoumia kwenye pambano la timu yake na Yanga, Novemba mwaka jana.

Simba ambao iliwaanzisha mabeki Ame Ibrahim na Pascal Wawa pamoja na Perfect Chikwende kikosi cha kwanza sambamba na Chama, Luis na Kagere, ilijikuta ikifungwa bao la pili dakika ya 76 kupitia Ayoub Lyanga aliyemalizia kazi nzuri ya ushirikiano kati ya Yahya Zayd na Nado aliyepiga krosi iliyomalizwa wavuni na mfungaji huyo likiwa bao lake la tano msimu huu.

Hata hivyo, bao hilo la Azam lilidumu kwa dakika mbili tu, kwani Luis alisawazisha akitumia pasi ya Chikwende aliyemzidi ujanja Obrey Chirwa ndani ya lango lao naye kufumua shuti kali lililomshinda nguvu Kigonya ambaye umahiri wake uliinyima Simba kutoka uwanjani na kapu na mabao.

Azam ilionekana kuwa imara kipindi cha pili kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Kocha George Lwandamina kwa kuwatoa Salum Abubakari na Ally Niyonzima nafasi zao zikichukuliwa na Yahya Zaid na Mudathir Yahya dakika ya 65 na kuifanya timu hiyo kuimarika zaidi.

Kocha Gomes naye alifanya mabadiliko ya kumtoa Perfect Chikwende na kuingia Benard Morrison kwa lengo la kwenda kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji, kabla ya kumtoa Bwalya ili kumpisha Chriss Mugalu na baadaye Luis alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mzamiru Yassin na Azam kumtoa Dube na kumwingiza Never Tigere.

Dakika tatu kabla ya kumalizika kwa pambano, Morrison aliikosesha Simba bao baada ya kupaisha mpira akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 39 kutokana na michezo 17, huku Azam ikifikisha pointi 33 baada ya mechi 18. Simba ina kiporo kimoja dhidi ya Namungo na kama itashinda itafanya pengo lao la pointi na vinara Yanga kusaliwa mbili.

NAMUNGO YAZINDUKA

Katika mchezo mwingine wa kiporo cha ligi hiyo uliopigwa Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi, wenyeji Namungo walizinduka kwa kuifumua Ruvu Shooting kwa mabao 2-1, bao la ushindi la timu hiyo likiwekwa kimiani dakika za jioni na Mghana Stephen Sey.

Awali Namungo walitangulia kupata bao dakika ya 63 na Jaffary Mohammed kabla ya Mwinyi Haji Mngwali kusawazisha dakika ya 89 na katika dakika za nyongeza Sey alikwamisha bao la ushindi la Namungo iliyotoka kufumuliwa mabao 3-0 na KMC katika mechi yao ya kiporo kilichopita.

Simba na Namungo zinajiandaa kuondoka kuanzia kesho kwenda Angola na DR Congo kwa mechi zao za kimataifa, Simba ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya As Vita na Namungo katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya 1st de Agosto.