Huu ndio utata safari ya ubingwa wa Yanga

Muktasari:
LIGI kuu ya Vodacom Tanzania Bara inafikia ukingoni mwezi huu huku bingwa wake akiwa ameshajulikana kabla ya michezo yote kumalizika. Huu ni mwendelezo wa jinsi bingwa wa Tanzania Bara amekuwa akipatikana mapema kabla ya siku ya mwisho ya michezo ya ligi kumalizika nadhani si chini ya misimu mitano au sita mfululizo sasa, hivyo klabu ya Yanga imerudia kufanya hivyo ikiwa ni kama utamaduni wa Tanzania katika soka la ushindani wa Ligi Kuu.
LIGI kuu ya Vodacom Tanzania Bara inafikia ukingoni mwezi huu huku bingwa wake akiwa ameshajulikana kabla ya michezo yote kumalizika. Huu ni mwendelezo wa jinsi bingwa wa Tanzania Bara amekuwa akipatikana mapema kabla ya siku ya mwisho ya michezo ya ligi kumalizika nadhani si chini ya misimu mitano au sita mfululizo sasa, hivyo klabu ya Yanga imerudia kufanya hivyo ikiwa ni kama utamaduni wa Tanzania katika soka la ushindani wa Ligi Kuu.
Kwa miaka takriban minne sasa ushindani wa kuwania nafasi ya bingwa wa nchi imebaki mikononi mwa timu mbili nchini za Yanga na Azam ingawa bado wamekuwa wakipata upinzani mkubwa kutoka kwa Simba ambayo ndani ya miaka hii minne imekuwa ikimaliza katika nafasi ya tatu na nne msimu wa 2013/2014.
Hata hivyo, ushindani wake umekuwa ukisuasua kwa misimu yote hiyo ya kuanzia 2012/2013 kwa bingwa na mshindi wa pili kuwaacha kwa mbali kwa pointi mapema ikiwa hata bado michezo mitano au minne kubakia, hali hiyo imekuwa ikitenganisha ubora wa Simba na timu hizo mbili za Azam na Yanga.
Hata hivyo, angalau hadhithi hiyo ilitaka kufutika katika msimu huu wa 2015/2016 baada ya Simba kuongoza ligi kwa muda mrefu huku ikiwa inafanikiwa kupata ushindi mfululizo wa michezo saba hadi kumi kitu kilicholeta matumaini ya kupatikana kwa bingwa mpya nje ya Azam na Yanga ambazo kwa pamoja zimepokezana kiti cha uongozi wa ligi toka ilipoanza.
Makala haya yanajaribu kugusia nini kilichozifanya timu hizi zifanikiwe kufika huku na kipi kilichoonekana kuwaharibia Simba na Azam kutofanikiwa kuchukua nafasi ya kwanza ya ubingwa wa nchi.
VIKOSI
Hapa ndipo safari ya mafanikio kwa timu zote tatu ilipoanzia kwa klabu zote kujiimarisha mapema katika Ligi Kuu ikiwa bado haijaanza, kulikuwa na sura nyingi mpya ndani ya Simba ukilinganisha na sura chache zilizoingia Yanga na Azam.
Sura mpya zilizoingia Simba zilikuwa 16 baadhi yao ni za Hamis Kiiza, Emiry Nimubona, Justice Majabvi na Vicent Angban, Pape Ndaw na Simon Serunkuma waliondolewa na kuletwa Brian Majwega na Rafael Kiongera hawa ni miongoni mwa wachezaji saba wa kigeni.
Wazawa ni Peter Mwalyanzi, Novatus Lufuga, Hadji Ugando, Mussa Mgosi, Danny Lyanga, Samih Nuhu, Mohamed Faki, Mwinyi Kazimoto na Joseph Kimwaga. Yanga waliwaleta wageni wawili kwanza Donald Ngoma na Thaban Kamusoko na baadaye wakaongezwa Vincent Bossou na Youssouf Boubacar aliyechukua nafasi ya Andrey Coutinho.
Iliwasajili wazawa saba Benedict Tinocco, Hadji Mwinyi,Geofrey Mwashiuya, Deus Kaseke, Malimi Busungu, Matheo Simon na Paul Nonga huku Azam ikiwa na idadi ndogo ya wachezaji wapya wageni watatu Allan Wanga, Jean Mugiraneza na Racine Diouf wazawa wakiwa ni Ramadhani Singano, Ivo Mapunda na Ame Ali.
Bila shaka ukiwachukua wachezaji wapya waliosajiliwa kwenye timu hizo tatu na kuwalinganisha kimizania utagundua kuwa pamoja na ubora wa wachezaji waliokuwapo kwenye timu hizo, Yanga ndiyo iliyofaidika na usajili mpya wa wachezaji sita kwa kujitokeza na kuwa muhimu katika kikosi chao, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Hadji Mwinyi, Vincent Bossou, Deus Kaseke na Geofrey Mwashiuya.
Simba inaweza kufuatia ikiwa na wachezaji wanne Hamis Kiiza, Mwinyi Kazimoto, Justice Majabvi na Vicent Angban.
Azam ikifaidika zaidi na Jean Baptiste Mugiraneza na Ramadhani Singano. Hata hivyo, bado Azam na Yanga zimeendelea kufaidika na uwepo wa wachezaji wazuri waliozoeana na kukaa pamoja kwa muda tofauti na Simba.
TAKWIMU
Takwimu mbalimbali ndizo zinazosababisha kuonesha kuwa, Yanga ilikuwa na kikosi bora uwanjani ukilinganisha na vikosi vya Azam na Simba. Kwanza kikosi cha Yanga kimeshinda michezo mingi zaidi na kwa idadi kubwa ya mabao 66, huku washambuliaji wake watatu Tambwe, Ngoma na Msuva wakiwa na mabao mengi kuliko ya washambuliaji wengine(45), wachezaji wa kati viungo licha ya kazi ya kuunganisha timu na kuichezesha nao wamehusika katika ufungaji wa mabao, Kamusoko na Kaseke wamefunga zaidi ya mabao matatu hata wachezaji wa nafasi ya ulinzi kama Kelvin Yondani na Juma Abdul wamefunga mabao ambayo si chini ya idadi hiyo (matatu).
Kikosi cha Yanga kimekuwa na wachezaji wanaojituma zaidi na kutokata tamaa hata pale timu yao inapokuwa imetanguliwa kufungwa, wamekuwa wakifanikiwa kusawazisha na kushinda mfano ni michezo dhidi ya Mwadui, Kagera, JKT Mgambo, Toto Africans na Prisons jijini Mbeya.
MATUMIZI YA UWANJA WA NYUMBANI
Kuufikia ubingwa wa nchi yoyote moja ya faida inayotakiwa kutumiwa na timu husika ni kunufaika kiufundi pale unapocheza nyumbani.
Msimu huu klabu ya Yanga imefanikiwa kushinda michezo 14 nyumbani na kutoa sare mchezo mmoja dhidi ya Azam na hivyo kujikusanyia jumla ya pointi 43, Azam inafuatia kwa kutumia vizuri kiasi uwanja wake wa nyumbani ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja huku ikivuna ushindi mara tisa na kutoa sare mara tano na kuvuna pointi 32.
Simba ikipoteza michezo minne na kutoa sare michezo minne katika uwanja wa nyumbani na kuvuna pointi 34. Matokeo haya yamesaidia zaidi kuzidhoofisha sa Azam na Simba katika kuukaribia ubingwa wa Tanzania Bara.
SIMBA ILIPOTEA MACHI 19
Ikiwa imetoka kushinda michezo isiyopungua minne mfululizo dhidi ya Mtibwa, Ndanda, Mbeya City na Prisons ilikwenda Tanga ikiwa na kauli mbiu ya kwamba mchezo dhidi ya Coastal ndiyo utakuwa wa mwisho kucheza na haitatokea uwanjani hadi pale timu za Azam na Yanga zitakapokuwa zimemaliza viporo vyao.
Hata hivyo, baada ya Simba kuishinda Coastal mjini Tanga kwa mabao 2-0 mchezo ukichezwa Machi 19, iliiandikia Bodi ya Ligi ikiitaka kuisogezea mbele michezo yake na bodi hiyo ilikubali kuipa likizo kwa jumla ya siku 24 ndani ya siku hizo kulikuwa na Sikukuu ya Pasaka ambayo wachezaji hawakuwa na jinsi zaidi ya kujilipua na kula raha huku wenzao wakiendelea na mashindano.
Ilikuwa ni kipindi ambacho Simba iliiacha ligi ikiwa inaongoza. Kukaa nje ya mashindano huku timu ikifanya mazoezi tu bila michezo ya ushindani kuliirudisha nyuma timu hiyo na kurudi kwao kulishuhudia anguko lao la kwanza kwenye michuano ya Kombe la FA, ikafuata kufanya vibaya kwenye michezo kadhaa na kwa haraka morali ya timu ikawa imepotea huku wachezaji wakionyesha viwango vibovu uwanjani.
AZAM JANUARI 27
Hii nayo ilikuwa moja kati ya programu mbovu za kimashindano ambayo klabu ya Azam iliamua kuifuata. Azam iliondoka nchini na kwenda Zambia kushiriki michuano ya ujirani mwema. Nadhani iliyozishirikisha timu nne tu za Zesco United na Zanaco kutoka Zambia, Chicken Inn ya Zimbabwe na wao Azam katika michuano iliyokuwa na dhana pamoja na uzito tofauti na Ligi Kuu yetu ya Vodacom.
Hayakuwa mashindano yaliyotakiwa kutumika na Azam katika kipindi ambacho Ligi Kuu ya Tanzania ilikuwa inaendelea, yalifaa sana kutumika mwanzoni mwa maandalizi ya msimu, ilikuwa ni kipindi hiki Azam ikaondoka nchini ikiwa ipo juu ya msimamo mwa ligi na pale iliporudi ilianza kuhangaika kurudia katika nafasi hiyo bila mafanikio.
ILIPOACHWA
Ilikuwa ni ratiba ngumu kwa Yanga na ratiba ya ajabu kutokea duniani kwa timu moja kuwa na michezo mitano mfululizo ugenini ama nyumbani kama ilivyowahi kuitokea timu ya Stand United ilipocheza michezo minne mfululizo ugenini.
Ratiba hii ilitoa ahueni mkubwa kwa klabu za Simba na Azam ambazo katika michezo hiyo mitano zilipangiwa michezo mitatu mitatu nyumbani na miwili ugenini, lakini katika hali ya kushangaza hadi sasa katika michezo hiyo mitano ya mwishoni kwa timu hizi tatu Simba imeshinda miwili ikapoteza miwili na kutoa suluhu mmoja na kupata pointi saba, Azam imepata pointi 11 baada ya kushinda mitatu na kutoa sare miwili wakati Yanga imeshinda michezo yote na kupata pointi 15 ambazo ziliwapandisha na kuwapa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya 26.
Bila shaka, timu zitajipanga kwa ajili ya msimu ujao na kujifunza kutokana na makosa ya msimu huu.