Hukumu ya Morrison yapasua vichwa

Benard Morrison

Muktasari:

Hukumu iliyotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imekuwa na mitazamo tofauti ya wadau.

Dar es Salaam. Hali imekuwa tofauti ikiwa ni siku moja baada ya hukumu ya hatma ya mshambiaji wa zamani wa Yanga, Benard Morrison kutoka.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilitoa uamuzi juzi kuwa nyota huyo ana kesi ya kujibu kwa Kamati ya Nidhamu licha ya kuonekana yuko huru kujiunga na timu yoyote aitakayo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya sheria, Elias Mwanjala akitoa hukumu ya Morrison juzi, alisema kulikuwa na mapungufu katika mkataba wa mshambuliaji huyo raia wa Ghana na Yanga, hivyo kuufuta mkataba huo na kumweka huru japo anatakiwa kwenda kwenye kamati ya nidhamu kwa kosa la kusaini mkataba mwingine (na Simba) wakati kesi yake ya usajili ikiwa inaendelea.

Lakini uamuzi na mlolongo mzima wa kesi hiyo imeleta taswira na mwonekano tofauti kwa wanasheria, ambao walikuwa wakiifuatilia kesi hiyo.

Wanasheria walikuwa na maoni tofauti juu ya jinsi ambavyo kesi hiyo imeamuriwa, huki kila mmoja akitoa mtazamo wake.

Wakili msomi Frank Chacha aliyewahi kuwa mwanasheria wa Yanga, alisema ameisikia hukumu hiyo na kutatizka na sababu zilizotolewa na kamati za kumweka huru Morrison.

“Kwa sababu hiyo kwanza, sijaona kosa ambalo limepelekea uonekane sio sahihi, sababu hiyo haisababishi mkataba kuwa halali, ni namna ya mtu anavyoamua kusaini ambayo sio shida kisheria.

“Mara kamati inasema, mkataba ulisainiwa tarehe ya nyuma na kuanza kufanya kazi tarehe ya mbele, hizo sababu sio za msingi hadi mkataba kuonekana kutokuwa na uhalali kisheria,” alisema Chacha.

Aliongeza kuwa, kuna sababu ambazo zinafanya mkataba ukose uhalali.

“Uwezo wa kusaini mkataba sheria inasema mtu awe na miaka 18 na kuendelea, mtu kasaini mkataba kwa kushawishiwa au awe kichaa au vinginevyo, au mkataba kwenda kinyume na sheria za nchi, hivi ni vitu vichache vya kusababisha mkataba kutokuwa halali,” alisema.

Chacha alisisitiza hadi kamati inatoa uamuzi yeye kama mbobezi katika masuala ya kisheria hajaona hoja za msingi ambazo zimetolewa juu ya malalamiko ya Yanga na Morrison.

Wakili msomi Joseph Singano aliyewahi kuhudumu ndani ya kitengo cha Sheria TFF, alishangazwa na hukumu ya kamati kwa kuwa ina mapungufu mengi, ambayo yanazua sintofahamu kwa wanamichezo hasa wapenz wa soka.

“Mkataba unatakiwa kuwa baina ya pande mbili, na uwe na makubaliano chanya, suala la mpira mikataba inakuwa na misimu na mkataba unaweza kuvunjwa kutokana na kiwango cha mchezaji mfano Samatta alivyotoka Simba kwenda TP Mazembe, ila hii ishu ya Morrison wanatakiwa waseme mkataba una mapungufu gani ambayo kisheria yameufanya mkataba huo kutokuwa halali kama ambavyo Yanga wanadai waliingia na mchezaji huyo,” alisema Singano.

Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Revocatius Kuuli alisema ushahidi uliotolewa una mashaka.

“Wanasema mkataba kama umegushiwa, mara kawa mchezaji huru, mara anapelekwa kamati ya maadili, sijawahi kuona mahakama haina hukumu ya kujitegemea hii ndio ya kwanza,” alisema Kuuli.

“Kama wanamashaka na mkataba hapo kunaonekana kuna jinai, sasa wametoaje uamuzi wakati inaonekana sintofahamu, huwezi kumwadhibu mtu kwa makosa ya mtu mwingine,”alisema Kuuli.

Deogratius Lyato aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, alisema, angeweza kutoa maoni yake juu ya hukumu hiyo lakini inakuwa ngumu kutokana na kutoiona nakala ya hukumu husika.