Hiki ndicho Kikosi bora cha wageni VPL 2019-20

Muktasari:

CLATOUS CHOTA CHAMA - Kiungo fundi asiye na mpinzani msimu huu wa VPL, amepiga asisti 10 na kufunga bao mbili

PAMOJA na kufanya vibaya kwa baadhi ya wenzao, hapana shaka idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni wamefanya vizuri katika Ligi Kuu msimu wa 2019/2020.

Wengi wameonekana kutoa mchango kwa timu zao na pengine bila juhudi zao, zisingeweza kuvuna pointi katika baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Makala hii inaangazia orodha ya nyota 11 wanaounda kikosi cha wachezaji bora wa kigeni katika Ligi Kuu ambao, mchango wao ilionekana kuwa mkubwa kulinganisha na wengine.

1. NURDIN BAROLA - NAMUNGO

Namungo FC ni miongoni mwa timu zilizoruhusu idadi ndogo ya mabao katika Ligi Kuu msimu huu, lakini pia imeweza kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi hiyo.

Uwepo wa kipa raia wa Burkina Faso, Nurdin Balora umechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya safu ya ulinzi ya Namungo kumudu mikiki ya washambuliaji wa timu pinzani.

Balora ana uwezo mkubwa wa kuokoa mashambulizi ya timu pinzani, kupanga timu, hesabu sahihi awapo langoni na pia mawasiliano mazuri na walinzi wake.

2. NICO WADADA - AZAM FC

Anashika nafasi ya pili kwa kupiga pasi nyingi za mwisho katika Ligi Kuu msimu huu akiwa nazo nane, pia amekuwa imara pia katika ulinzi.

Pamoja na kutamba katika kupika mabao, Wadada pia amefunga bao moja katika Ligi Kuu msimu huu na pindi anapokosekana, Azam imekuwa ikitetereka katika upande wake.

3. BRUCE KANGWA - AZAM FC

Katika umri wa miaka 31, Bruce Kangwa ameendelea kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Azam kutokana na mchango wake kwenye timu hiyo.

Uwezo wake katika kukaba, kupandisha mashambulizi na upigaji mipira iliyokufa na kona, umekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo msimu huu.

4. LAMINE MORO - YANGA

Kwa muda mrefu, safu ya ulinzi ya Yanga ilikuwa inamkosa beki wa kati kiongozi, lakini pengo hilo linaonekana kuzibwa vyema na Mghana Lamine Moro, ambaye amekuwa muhimili imara wa safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Licha ya kucheza na kundi kubwa la mabeki wenye kiwango cha wastani, Moro amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga msimu huu na anapokosekana timu hiyo imekuwa ikifanya vibaya zaidi katika ulinzi.

5. SERGE WAWA - SIMBA

Simba haikukosea kumpa mkataba mpya beki Serge Wawa ili aendelee kuitumikia timu hiyo msimu huu.

Uwezo wake wa kusoma na kudhibiti mikimbio ya washambuliaji wa timu pinzani, kuwasiliana vyema na walinzi wenzake na kuchezesha timu kuanzia nyuma, kumemfanya awe na namba ya kudumu katika kikosi cha Simba msimu huu.

6. GERSON FRAGA - SIMBA

Safu ya ulinzi ya Simba imekuwa salama zaidi pindi Mbrazil, Gerson Fraga anapokuwa uwanjani kutokana na uwezo wake wa kutibua na kuvuruga mashambulizi na mipango ya timu pinzani na kuchezesha timu.

Lakini, pia ameonyesha uwezo wa kufumania nyavu pindi anapolisogelea lango la timu pinzani na kudhihirisha hilo, ameifungia Simba, mabao matatu kwenye Ligi Kuu.

7. LUIS MIQUISSONE - SIMBA

Alijiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili, lakini ndani ya muda mfupi ameweza kugeuka tishio kwenye ligi na kutoa mchango mkubwa kwa timu yake.

Mabao manne aliyofunga na pasi tano za mabao alizopiga ni ishara tosha ya mchango wa Miquissone alioutoa kwa Simba ndani ya muda mfupi.

8. CLATOUS CHAMA - SIMBA

Jukumu kuu la kiungo mshambuliaji ni kuzalisha mabao iwe kwa kufunga ama kupiga pasi ya mwisho.

Mzambia Clatous Chama ameendelea kudhihirisha kuwa hana mpinzani katika hilo kwani, ndiye kinara wa kupiga pasi za mwisho katika Ligi Kuu msimu huu.

Kiungo huyo kabla ya mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Polisi Tanzania, alikuwa amepiga pasi 10 za mabao huku pia akiifungia Simba, mabao mawili.

9. MEDDIE KAGERE - SIMBA

Kwa msimu wa pili mfululizo, Meddie Kagere ameendelea kuwa tishio katika kufumania nyavu, akirudia kile alichokifanya msimu uliopita ambacho ni kumaliza msimu akiwa mfungaji bora.

Mabao yake 22 yamemfanya awe mfungaji bora wa ligi kuu kwa mara ya pili mfululizo kama alivyofanya msimu uliopita alipopachika mabao 23.

10. OBREY CHIRWA - AZAM FC

Mabao 12 aliyofunga na pasi nne za mwisho alizopiga msimu huu ni ishara tosha ya jinsi Chirwa alivyoweza kutunza makali yake na kuendelea kuwa msaada kwa kikosi cha Azam msimu huu.

Achana na idadi hiyo ya mabao aliyopachika, lakini pia anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao matatu (hat trick) katika mchezo mmoja mara nyingi akifanya hivyo mara mbili katika mechi mbili za Azam dhidi ya Alliance na Singida United.

11. DEO KANDA - SIMBA

Licha ya kucheza nafasi ya winga, Kanda ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao kulinganisha na wachezaji wengine wanaocheza katika nafasi hiyo.

Licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha Simba, Kanda amefunga jumla ya mabao nane (8) katika Ligi Kuu huku pia akipiga pasi mbili (2) zilizozaa mabao msimu huu.

KOCHA HITIMANA - NAMUNGO

Kocha Thierry Hitimana wa Namungo, ndiye anayeingia kwenye orodha hii ya skwadi la mapro wa kigeni kutokana na kile alichokifanya kwa timu hiyo iliyopanda msimu huu na kumaliza nafasi nne ya katika msimamo, huku ikitinga pia fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) inayopigwa Jumapili dhidi ya Simba.

Kocha huyo ameifanya Namungo kuwa tishio msimu huu ikipata matokeo ya kushangaza hata kwa vigogo licha ya ugeni wake katika ligi hiyo.

WALE WA AKIBA

Kila kikosi huwa na nyota wa akiba na katika orodha hii wapo wachezaji kadhaa akiwamo kipa Razack Abarola wa Azam, Yakub Mohammed (Azam) Papy Tshishimbi (Yanga), David Molinga (Yanga), Never Tigere (Azam), Steve Opoku (Singida United), Blaise Bigirimana (Namungo) na Raphael Aloba (Mwadui).