Mkomola kambi kokote, apiga mkwara

Muktasari:
- Nyota huyo amejiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) katika dirisha dogo la Januari mwaka huu 2025, na kusaini mkataba wa miaka miwili, akitokea Songea United ya mkoani Ruvuma inayocheza Ligi ya Championship msimu huu.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga na Tanzania Prisons, Yohana Mkomola anayekipiga kwa sasa KVZ amesema kitendo cha kujiunga na timu hiyo kimempa motisha kubwa ya kurejea katika kiwango chake msimu huu, baada ya kuanza vibaya kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.
Nyota huyo amejiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) katika dirisha dogo la Januari mwaka huu 2025, na kusaini mkataba wa miaka miwili, akitokea Songea United ya mkoani Ruvuma inayocheza Ligi ya Championship msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkomola alisema baada ya kupata nafasi hiyo aliamua kubadilisha mazingira ili kujitafuta tena upya, hivyo anashukuru tangu amejiunga na kikosi hicho amepata sapoti ya kutosha na amerejea katika kiwango anachopenda.
“Ligi ya Zanzibar ni ngumu kama ilivyo pia ya Bara, nimeanza maisha mapya na kiukweli hadi sasa nashukuru kuona kile nilichokitarajia kukifanya kwa ubora kinaenda vizuri, licha ya kuanza msimu huu na timu hii katikati,” alisema.
Kabla ya Songea United, nyota huyo alitokea Tabora United, huku akizichezea Yanga, Tanzania Prisons za Tanzania na FC Vorskla Poltava, FK Girnyk-Sport Gorishni Plavni na Ingulets Petrove za Ukraine na Etoile du Sahel (U-19) ya Tunisia.
Akiwa na kikosi hicho cha KVZ kilichoshiriki michuano ya Kombe la Muungano mwaka huu wa 2025 na kutolewa na Yanga baada ya kuchapwa mabao 2-0, katika hatua ya robo fainali, amecheza mechi 11, ambapo amefunga mabao matano na kuasisti mawili.
Katika ZPL, KVZ inashika nafasi ya nne katika msimamo kwa pointi 47, baada ya kucheza mechi 25, ambapo kati ya hizo imeshinda 12, sare 11 na kupoteza mbili, ikifunga mabao 24 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.
Mwembe Makumbi City ndiyo inayoongoza ikiwa na pointi 49, ikifuatiwa na Mafunzo inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 48, huku Mlandege ikiwa ya tatu kwa pointi 47 sawa na KVZ ya nne zikitofautiana mabao, baada ya timu zote kucheza mechi 25.