Laizer atwishwa zigo Fountain Gate

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer alisema hahofii masharti aliyopewa kutokana na kuamini timu hiyo inaweza kujinasua katika janga la kushuka daraja, huku akiwaomba mashabiki, wachezaji na viongozi kiujumla kushikamana kwa mechi zilizobakia.
KOCHA mpya wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’, amefikia makubaliano ya kukiongoza kikosi hicho katika mechi mbili zilizobakia msimu huu, huku akiweka wazi sharti kubwa alilopewa ni kuhakikisha timu hiyo inabakia Ligi Kuu msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer alisema hahofii masharti aliyopewa kutokana na kuamini timu hiyo inaweza kujinasua katika janga la kushuka daraja, huku akiwaomba mashabiki, wachezaji na viongozi kiujumla kushikamana kwa mechi zilizobakia.
“Nimerejea kwa mara ya pili, lakini kwangu hainishtui kwa sababu ndio kazi zetu zilivyo, leo upo hapa na kesho unaweza kuangukia kwingine, lengo la timu ni kubaki Ligi Kuu msimu ujao na hicho ndicho tunachokipambania sasa,” alisema Laizer.
Kocha huyo kwa sasa atafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Mkurugenzi wa Ufundi, Melis Medo aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Singida Black Stars, ikiwa ni muda mfupi tangu avunje mkataba na Kagera Sugar ambayo tayari imeshashuka daraja.
Laizer amejiunga na timu hiyo baada ya kuondoka kwa makocha wa kikosi hicho kwa sasa, Khalid Adam na Amri Said ‘Stam’, ambao pia waliachiwa kutokana na kitendo cha aliyekuwa kocha mkuu, Mkenya Robert Matano kuvunja mkataba kikosini.
Hii ni mara ya pili kwa Laizer kurejea katika timu hiyo baada ya kuanza nayo msimu akiwa ni kocha msaidizi wa Mohamed Muya ambao waliondoshwa kikosini Desemba 29, 2024, ikiwa ni muda mchache kutokana na kuchapwa mabao 5-0, dhidi ya Yanga.
Kichapo hicho ndicho kikawaondoa makocha hao, ambapo Muya alijiunga na Geita Gold huku kwa upande wa Laizer akajiunga na TMA Stars ya jijini Arusha zote zikiwa zinashiriki Ligi ya Championship msimu huu uliotamatika rasmi Mei 11, 2025.
Akiwa na TMA, Laizer alikuwa kocha mkuu baada ya Maka Mwalwisi kuondoka na kujiunga na Mbeya Kwanza, huku akiiwezesha kumaliza katika nafasi ya tano kwa pointi 53, baada ya kushinda mechi 15, sare nane na kuchapwa saba.
Fountain Gate inayoshika nafasi ya 14 kwa pointi 29, baada ya kucheza mechi 28 ikishinda nane, sare tano na kupoteza 15, ni timu inayoongoza kuruhusu mabao mengi katika Ligi Kuu Bara, ikifungwa 54, ikifuatiwa na KenGold iliyoruhusu 52.
Timu hiyo imesaliwa na mechi mbili dhidi ya Coastal Union ya Juni 18 ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kumalizia na Azam Juni 22 kwenye Uwanja Tanzanite Kwaraa, mjini Babati, Manyara.