Hearn amhofia AJ kwa Usyk

Wednesday January 12 2022
AJ PIC
By Matereka Jalilu

ANTHONY Joshua ‘AJ’, bondia wa uzito wa juu duniani kutoka England anahesabu miezi mitatu kuanzia sasa kabla hajapanda ulingoni kukomboa mikanda yake mitatu aliyokuwa nayo - IBF, WBA, na WBO baada ya kukutana na kitu kizito kwa kukalishwa na Oleksandr Usyk.

Usyk anayetokea nchini Ukraine alifanikiwa kumchapa AJ kwa pointi tena akiwa kwenye ardhi ya nyumbani kwao pale London, Uingereza, akishinda kwa ushindi wa majaji wote watatu katika pambano lililofanyika uwanjani Tottenham.

Mwezi Aprili, mwaka huu, bondia huyo anatakiwa kupambana kurudisha mikanda hiyo iliyopo mikononi mwa Usyk, jambo lililomfanya afanye uamuzi unaoonekana kumtia wasiwasi promota wake Eddie Hearn wa kampuni ya Matchroom.

Hearn, amekuwa na shaka kubwa kwa kitendo cha AJ kumtema mkufunzi wa miaka yote Rob McCracken kisa tu ameshauriwa na wadau tofauti kwamba anatakiwa asake mkufunzi wa kumpa mbinu nyingine, jambo ambalo limemuingia bondia huyo, lakini Hearn amekuwa na shaka kubwa.

Eddie Hearn anaamini mteja wake amefanya uamuzi unaotia wasiwasi akitambua kuwa kubadilisha kocha ikiwa ni miezi mitatu kabla ya kurudiana na Usyk inaweza kumgharimu.

Advertisement