Hatma ya Lamine mikononi mwa mabosi wake

TANGU aliporudishwa Dar es Salaam, wakati Yanga ikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo wiki iliyopita, bado haijulikani nini hatima ya nahodha Lamine Moro.
Licha ya Lamine mwenyewe kukaririwa kuwa kurudishwa kwake Dar es Salaam haikuwa kwa sababu za utovu wa nidhamu, lakini taarifa zinadai kwamba ni kutokana na hilo na hivyo ili arudishwe kundini itachukua muda.
Suala lake la kurejea kikosini wakati ambao timu hiyo inapambania kusaka matokeo ili kuona kama itabeba ubingwa wa ligi hiyo unaowaniwa pia na Simba, bado halijafanyiwa kazi.
Hii inamaanisha kwamba hatima nzima ya nahodha huyo wa Yanga haijawa tayari hadi pale atakaporudishwa katika kikosi cha timu hiyo kumalizia mechi zilizobaki na ule mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Mwadui.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Dominick Albinus alipoulizwa juu ya beki huyo alisema kuwa: ‘‘Lamine hayupo kwenye kundi la wachezaji waliokuja Dodoma, kuhusu suala lake bado halijamalizika ambapo sekretarieti ya timu itakaa na kuamua maamuzi ya mwisho juu yake.”