Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hata Rais Trump atamuonea huruma Mkwasa

Muktasari:

  • Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ana hali ngumu ndani ya timu hiyo. Ametimiza mechi 13 katika timu ya taifa na ameshinda michezo miwili tu.

DONALD Trump. Mtu mmoja mwenye roho ya chuma. Mtu mmoja mwenye moyo wa uvumilivu na asiyekata tamaa. Akitaka kitu lazima akipate. Ameutaka urais wa Marekani na akaupata, licha ya kukatishwa tamaa kila kona.

Trump wakati wa kampeni alisalitiwa na watu wa chama chake, watu wake wa karibu na dunia pia. Alijiunga mkono mwenyewe pamoja na watu wachache waliokuwa nyuma yake. Ni binadamu wachache wenye ujasiri huo.

Kwa kifupi Trump ni mtu mmoja mwenye moyo mweusi na anatisha. Alipotangazwa tu kuwa rais, maelfu ya Wamarekani walijitokeza barabarani wakiandamana kumpinga. Anaonekana pia ni mtu wa maamuzi magumu.

Katika kizazi cha sasa, Trump anaweza kuwa binadamu mwenye sifa nyingi zaidi. Ana sifa zote za kuwa katili. Ana sifa zote za kuwa mpole na mwenye busara. Miongoni mwa misimamo yake ni kwamba viongozi wa Afrika wanalegalega sana na wanatakiwa kuamshwa.

Ni kama tunavyoamini kuwa Jamal Malinzi ameishindwa TFF. Ni kama tunavyoamini Tanzania ni maskini kutokana na uwepo wa viongozi wabovu. Ni kama tunavyoamini kuwa Taifa Stars imegota mahali kutokana matatizo yetu wenyewe.

Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ana hali ngumu ndani ya timu hiyo. Ametimiza mechi 13 katika timu ya taifa na ameshinda michezo miwili tu. Hata hivyo, mchezo mmoja ulifutwa ambao ni dhidi ya Chad na sasa ni sawa na ameshinda mchezo mmoja tu ambao ulikuwa dhidi ya Malawi mwaka jana.

Katika kipindi cha Mkwasa tumecheza na Kenya tukashindwa kuifunga. Tukacheza na Uganda tukashindwa kuifunga. Tukacheza na Zimbabwe na Libya tukashindwa kuzifunga. Si vizuri kuzungumzia habari za kutisha za kipigo cha Algeria. Ni maisha magumu kwa kocha yeyote.

Hata hivyo, Mkwasa amebaki tu kama chambo kwa sasa. Malinzi amejificha nyuma ya Mkwasa. Matatizo yetu tumeyaficha pia nyuma ya Mkwasa. Mzigo wote inabidi aubebe Mkwasa hata kama siyo kosa lake. Hata hivyo, ukiyatazama matatizo ya soka letu utamwonea huruma Mkwasa. Hata Trump pia anaweza kumwonea huruma.

Tuanze kutazama matatizo madogo tu ambayo yameambatana na Taifa Stars.

Hivi majuzi timu ikiwa inasafiri kwenda Zimbabwe wachezaji watano waliachwa kutokana na kukosa hati za kusafiria (passport).

Mchezaji kama alikuwa na mpango wa kujumuishwa kwenye timu ya taifa kwa nini hakutafutiwa hati ya kusafiri mapema? Sidhani kama Mkwasa ndiye anayetakiwa kujibu swali hilo?

Mkwasa hajalipwa mishahara yake na hana pia bajeti ya kwenda kusaka wachezaji katika mechi za mikoani.

Ameishia kuwa kocha wa Dar es Salaam na anashinda katika ofisi za TFF na kwenda kutazama mechi zinazochezwa jijini hapo. Nimesafiri na timu kwenda Mbeya na Shinyanga sikumwona Mkwasa.

Nimefuatilia mechi nyingi zinazochezwa nje ya Dar es Salaam kupitia Azam TV, lakini sikumuona Mkwasa. Kama hajapewa bajeti ya kusafiri mikoani kutazama wachezaji wenye uwezo wa kuisaidia timu ya taifa napo tumlaumu?

Ukiachana na hayo, soka letu limegubikwa na tuhuma za rushwa. Leo hii imefikia hatua hadi Majimaji ya Songea inatuhumiwa kutaka kununua mechi. Kama hadi Majimaji inapata tuhuma za kutaka kupata matokeo kwa njia isiyo halali ni nani atasalimika?

Ligi inapungua msisimko kutokana na kuwepo kwa tuhuma za rushwa. Wachezaji wanacheza uongo uongo kutokana na kuwepo kwa madai ya rushwa. Mwishowe Mkwasa anaita wachezaji wenye uwezo wa uongo ambao wanaishia kulidanganya taifa.

Ukiachana na hilo, bado uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa taifa wa sasa umeachwa mbali na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja katika miaka mitano ama minane iliyopita. Pengine Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaweza kwenda sawa na wachezaji waliokuwepo kabla. Leo hii Saimon Msuva bado hajafikia ubora wa Mrisho Ngassa wa miaka mitano nyuma. Shiza Kichuya bado hajaukaribia uwezo wa Ulimboka Mwakingwe. Himid Mao na Jonas Mkude bado hawajafikia uwezo wa Athuman Iddi ‘Chuji’.

Je, utaweza kumfananisha Ibrahim Ajibu na Haruna Moshi Boban? Ama unaweza kumfananisha Elias Maguli na Mussa Hassan ‘Mgosi’? Hebu tazama vizuri kama tunaweza kumfananisha Mzamiru Yassin na Henry Joseph aliyekuwepo katika ubora wake.

Huwezi kumfananisha Andrew Vincent na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ au Juma Nyosso wa miaka mitano iliyopita. Uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa sasa ni mdogo kuliko wa wachezaji wa miaka mitano au saba iliyopita.

Hata hivyo, kama miaka hiyo tulikuwa na wachezaji wazuri, Kocha Mbrazili, Marcio Maximo na TFF imara ya Leodger Tenga na hatukuweza kufanya maajabu zaidi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan), Mkwasa leo ataweza kufanya kitu gani kipya?

Ukichukua taarifa hizi za mpira wa Tanzania halafu na matokeo ya Mkwasa ukazipeleka kwa Donald Trump ni dhahiri kuwa atamwonea huruma. Ataona namna anavyofanya kazi katika mazingira yaliyokufa. Ataona namna ambavyo hakuna kocha ambaye ataweza kututoa hapa tulipo kwenda kwingine.

Kama hatutaziba mianya ya rushwa kwenye mpira wetu. Kama hatutakuwa na TFF imara. Kama hatutakuwa na ligi yenye ushindani wa kutosha na kama hatutauza wachezaji wengi zaidi kwenda kucheza nje, hatutaweza kutoka hapa tulipo kwenda hatua nyingine. Ni sawa na kuendelea kuamini kuwa umaskini utaisha Tanzania.

Kama tumeshindwa katika riadha. Kama tumeshindwa katika kuogelea na masumbwi. Kama tumeshindwa katika michezo mingine yote basi angalau tuwekeze nguvu katika soka. Basi tujitahidi kuwekeza kwenye soka kwa kiwango cha juu zaidi ili tusonge mbele kama taifa.