Hat trick ya Aziz KI yafikia rekodi tamu

Muktasari:
- Katika historia ya soka la Bongo, Abdallah Kibadeni pekee ndiye mchezaji aliyewahi kufunga hat trick kwenye mchezo wa dabi akifanya hivyo Julai 19,1977 Simba ikiichapa Yanga mabao 6-0.
JUA liwake, mvua inyeshe lazima kieleweke wikiendi hii pale kwa Mkapa wakati Simba na Yanga zitakapovaana kwenye mchezo wa Ligi Kuu huku mchezo wa duru ya kwanza ziligawana alama baada ya sare ya bao 1-1.
Katika historia ya soka la Bongo, Abdallah Kibadeni pekee ndiye mchezaji aliyewahi kufunga hat trick kwenye mchezo wa dabi akifanya hivyo Julai 19,1977 Simba ikiichapa Yanga mabao 6-0.
Tukiachana na mambo ya dabi katika misimu minne ya Ligi Kuu msimu wa 2019/20 ndio unashikilia rekodi ya kuwa na hat trick nyingi (7), lakini ghafla mambo yamebadilika msimu huu.
Hat trick ya Aziz Ki dhidi ya Kagera Sugar imefanya msimu kufikisha idadi ya hat trick saba huku michezo ikisalia mitano ili msimu kufikia mwisho, lakini ikiongeza utamu ya kuwa mchezaji wa nne wa kigeni kutupia akifunika rekodi ile ya msimu wa 2019-2020.
Katika hat trick saba za msimu huo, nyota wa kigeni walikuwa wawili tu, Obrey Chirwa na Meddie Kagere, huku waliosalia wakiwa wazawa, lakini safari hii wageni ni wanne na wawili wakiwa wazawa akiwamo Bocco alifeunga hat trick mbili.
Bocco anayekipiga Simbaalifunga hat trick ya kwanza Novemba 19 wakati Simba ikiichapa Ruvu Shooting 4-0 na Desemba 30 akapiga hat trick yake ya pili kwenye ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Prisons ambapo mchezo huo ulizamisha hat trick mbili ikiwamo ya Saido Ntibazonkiza aliyekuwa akiichezea Simba kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe kutoka Geita Gold.
Hat trick nne kati ya nne kati ya saba za msimu huu zimefungwa Uwanja wa Mkapa, huku ya kwanza ikiwa Novemba 17 ile ya Fiston Mayele (Yanga) walipoichapa Singida 4-1.
Nyota mpya wa Namungo, Ibrahim Mkoko ndiye mchezaji nje ya Simba na Yanga msimu huu kupiga hat trick katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KMC Uwanja wa Uhuru na saba ile ya Jean Baleke dhidi ya Mtibwa Uwanja wa Manungu Machi 11,2023.
Msimu uliopita kulikuwa na hat trick tatu ile ya Jeremiah Juma (Prisons) Uwanja wa Nelson Mandela ilipoichapa Namungo mabao 3-1, Shiza Kichuya wakati Namungo ikiichapa Mtibwa 4-2 na Idrisa Mbombo, Azam ikiifunga Biashara 4-1.
Msimu wa 2020/21 nako kulikuwa na hat trick tatu ile ya Adam Adam wakati JKT Tanzania ikiichapa 6-1 Mwadui FC, Bocco wakati Simba ikiisambaratisha Coastal Union mabao 7-0 na Juma Liuzio wakati Mbeya City ikiifunga 4-0 Biashara United.
Hat trick saba za msimu wa 2019/20 ya kwanza ilikuwa ya Ditram Nchimbi wakati akiwa Polisi Tanzania ilipovaana na Yanga Uwanja wa Uhuru Oktoba 3 na timu hizo kutoka sare ya bao 3-3.
Wachezaji wengine waliofunga hat trick ni Daruwesh Saliboko (Lipuli FC) ilipoichapa 5-1 Singida United Uwanja wa Samora, Iringa, Obrey Chirwa wa Azam FC ikiifunga 5-0 Alliance FC.
Kelvin Sabato (Kagera Sugar) alifanya hivyo walipoisambaratisha 3-0 Singida United pale Kaitaba, David Richard wa Alliance FC naye aliingia kwenye kitabu hicho alipofanya yake wakati wakiichapa 4-1 Mwadui FC.
Meddie Kagere (Simba) naye alifanya hivyo walipoisambaratisha 8-0 Singida United alipotupia bao nne kambani. Mchezaji wa mwisho kufunga hat trick msimu huo alikuwa, Atupele Green (Biashara) walipoichapa 4-0 KMC.
Kama kasi ya kutupia itaendelea kwa mechi za raundi nne zilizosaliwa kabla ya ligi kufikia tamati huenda hat trick zinaongezeka na kuweka rekodi ya kipekee katika Ligi Kuu kwa miaka ya karibuni.