HAPAPITIKI KIRAHISI : Angalia safu za viungo wa timu hizi za Ligi kuu

Jonas Mkude
Muktasari:
Anapokosekana kiungo wao, Salum Telela hali inakuwa mbaya kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara. Mbuyu Twite anayechezeshwa katika nafasi ya kiungo mkabaji ameshindwa kuimudu nafasi hiyo vizuri.
YANGA ina safu laini zaidi ya kiungo ukilinganisha na Azam na Simba. Timu hiyo imeimarika zaidi katika safu ya ushambuliaji na ulinzi lakini katikati bado ni shida.
Anapokosekana kiungo wao, Salum Telela hali inakuwa mbaya kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara. Mbuyu Twite anayechezeshwa katika nafasi ya kiungo mkabaji ameshindwa kuimudu nafasi hiyo vizuri.
Ukiacha Yanga ambayo ina safu laini kidogo ya kiungo, kuna timu kadhaa za Ligi Kuu ambazo safu zao za kiungo ni hatari. Zimejaa vijana mahiri ambao kazi zao hazina mashaka kabisa.
Makala haya yanakuletea orodha ya timu za Ligi Kuu ambazo kama utakutana nazo ni vyema ukapandisha mashambulizi kupitia pembeni maana katikati ni pagumu kupitika pengine kuliko safu nyingine zozote za timu hizo.
Azam
Matajiri wa Bara, Azam wanaweza kuwa timu yenye safu ngumu zaidi ya kiungo. Timu hiyo ina viungo sita tofauti ambao wakicheza dimba la kati, basi shughuli yake inakuwa pevu.
Timu hiyo ina Frank Domayo, Himid Mao, Kipre Bolou, Mudathir Yahya, Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ na Salum Abubakar ‘Sure Boy’. Mbali na hao pia Azam ina mkongwe Erasto Nyoni ambaye pia anamudu kucheza nafasi ya kiungo.
Viungo hao wote wa Azam ni wa viwango vya juu, wote ni wazuri katika kukaba na kupandisha timu. Kocha Stewart Hall amekuwa akiwatumia viungo watatu kwa pamoja jambo ambalo linazipa shida timu pinzani.
Mwadui
Hii ni timu mpya Ligi Kuu lakini usajili iliyofanya unaonekana kabisa kuipa timu hiyo kiburi katika safu yake ya kiungo. Mwadui ina viungo watano mahiri wenye uzoefu na Ligi Kuu huku pia ikiwa na viungo wengine chipukizi. Safu ya kiungo ya Mwadui inaundwa na mkongwe, Athuman Iddi ‘Chuji’, Jabir Aziz ‘Stima’, Anthony Matogolo, Nizar Khalfan na Jamal Mnyate.
Uwepo wa Chuji, Stima na Matogolo kwa pamoja katika timu hiyo ni ishara kuwa timu pinzani zijiandae kupita pembeni. Viungo hao wote watatu ni wazuri katika kukaba, wanapiga pasi makini na za uhakika. Ni vigumu sana kutawala dimba la kati mbele ya watatu hao.
Simba
Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, Simba wamemrejesha kundini kiungo wao wa zamani, Mwinyi Kazimoto. Uwepo wa Kazimoto katika kikosi cha Simba ni ishara kuwa timu hiyo itakuwa na safu ngumu pia ya kiungo.
Mbali na Kazimoto Simba ina Jonas Mkude, Abdi Banda na Said Ndemla ambao ni mahiri pia katika dimba la kati. Mkude na Banda ni wazuri katika kukaba na wanapandisha timu kama ilivyo kwa Kazimoto.
Ndemla licha ya kuchezeshwa kama kiungo mchezeshaji pia ni mzuri katika kukaba. Timu hiyo pia ina Peter Mwalyanzi ambaye anamudu pia kucheza nafasi ya kiungo hivyo kuifanya safu yao iwe imara zaidi.
Mtibwa Sugar
Pia ni mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, walikuwa na safu imara zaidi ya kiungo msimu uliopita. Msimu huo Mtibwa ilikuwa na Mussa Nampaka, Henry Joseph, Jamal Mnyate, Ibrahim Jeba, Mohammed Ibrahim na Mkongwe Shaban Nditi ambao wote walionyesha kiwango cha juu.
Msimu huu ni Mnyate pekee aliyepungua katika safu hiyo jambo ambalo haliachi pengo lolote. Nditi anaendelea kuwa nguzo katika timu hiyo licha ya umri wake kusonga na amekuwa akiwapa tabu viungo wa timu pinzani.
Uwepo wa Henry Joseph pia unaipa uimara zaidi Mtibwa kutokana na soka lake maridadi, uwezo wake wa kukaba na kupiga pasi za uhakika japo si kama alivyokuwa miaka mitatu iliyopita.
Mbeya City
Timu hii inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya haitishi tena kama ilivyokuwa katika msimu wake wa kwanza lakini bado inaendelea kuwa na safu imara ya kiungo. Katika kipindi cha miaka miwili timu hiyo imeondokewa na nyota zaidi ya 10 lakini haijaathirika sana katika eneo la kati.
Usajili mpya wa Joseph Mahundi kutoka Coastal Union na uwepo wa viungo wengine klabuni hapo kama Ken Ally, Raphael Alfa na Steven Mazanda unaifanya timu hiyo iendelee kuwa na safu imara ya kiungo.
Ni dhahiri kuwa timu zitakazokutana na Mbeya City zijiandae kupenya kupitia pembeni.