Hakim Ziyech fundi wa asisti aliyetua Chelsea mapema tu

Muktasari:

Lakini, kwa nini Chelsea imeamua kumaliza usajili wa Ziyech mapema hivi? Ni nani huyu jamaa? Na mashabiki wa miamba hiyo ya Stamford Bridge watarajie nini kutoka kwake? Hayo ni baadhi ya maswali yatakayojibiwa na safu hii.

LONDON, ENGLAND. WAKATI timu nyingine zikisubiri msimu uishe ndiyo zianze kukimbizana kwenye soko la usajili, Chelsea haijataka kuremba, mapema tu imemaliza shughuli kwa Hakim Ziyech.

Baada ya kushindwa kusajili mchezaji hata mmoja Januari, Chelsea sasa imeamua kutumia msemo wa ‘biashara asubuhi, jioni mahesabu’ na ndiyo maana mapema imemalizana na Ajax kwa Ziyech na sasa staa huyo atatua Stamford Bridge mwisho wa msimu kwa Pauni 37 milioni.

Lakini, kwa nini Chelsea imeamua kumaliza usajili wa Ziyech mapema hivi? Ni nani huyu jamaa? Na mashabiki wa miamba hiyo ya Stamford Bridge watarajie nini kutoka kwake? Hayo ni baadhi ya maswali yatakayojibiwa na safu hii.

Ni Nani?

Hakim Ziyech alizaliwa Machi 19, 1993, katika mji wa Dronten, Uholanzi akiwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto tisa, wa kiume watano na wa kike wanne.

Maisha yake hayakuwa rahisi utotoni kwa sababu baba yake alifariki wakati Ziyech akiwa na umri wa miaka 10 tu, hivyo yeye na ndugu zake walilelewa na mama yao peke yake.

Utotoni alijiepusha na majanga pamoja na magenge ya kihuni kwa kucheza soka, licha ya kuwa na umri pamoja na umbo dogo - alicheza na watu wakubwa huku akiwa na uwezo mkubwa sana wa kupiga chenga kitu kilichompa umaarufu katika viwanja vya mchangani.

Maisha ya soka

Alianza maisha ya katika akademi ya Real Dronten mwaka 2001, kisha baadaye akahamia ASV Dronten kabla ya 2007 kujiunga na akademi ya Heerenveen.

Akademi ya Heerenveen ilimnasa akiwa na miaka 14, kisha akalazimika kutumia miaka sita kupambana kuingia kwenye kikosi cha kwanza ambapo alifunga mabao 11 katika mechi 36 za msimu wa 2013-14.

Kiwango hicho kilimfanya aonwe na FC Twente ambako ndiko alijijengea jina zaidi ndani na nje ya Uholanzi.

Mabao 11 na pasi za mabao 16 msimu wa kwanza yalifuatiwa na mabao 17 na pasi za mabao 10 msimu uliofuata.

Katika msimu wake wa pili Twente alipewa kitambaa cha unahodha, lakini alivuliwa miezi sita baadaye baada ya kutoa maneno ya dhihaka dhidi ya uongozi wa klabu hiyo huku akisisitiza alikuwa anataka kuondoka.

Ziyech alishambulia kila kitu kuhusu klabu hiyo na jinsi ilivyokuwa inaendeshwa baada ya kutimuliwa kwa kocha Alfred Schreuder. Mashambulizi yake kwa uongozi wa klabu yaliendelea kiasi cha kushauriwa kuacha kuongea na vyombo vya habari.

Licha ya kuongea sana, lakini uwanjani pia Ziyech aliendelea kufanya vizuri kiasi cha kuivutia Ajax, kumsajili Agosti 30, 2016, aliendelea kufanya vizuri Ajax katika msimu wake wa kwanza akifunga mabao 12 na kutoa pasi za mabao 20 na kuiongoza timu hiyo hadi fainali ya Europa League ilipofungwa 2-0 na Manchester United.

Ujio wa Erik ten Hag mwaka 2017 ulimsaidia kupandisha kiwango chake zaidi, ambapo katika msimu wa 2018-19, timu hiyo ilifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, huku Ziyech akifunga mabao 19 na kupiga pasi za mabao 17 katika michuano yote msimu huo.

Msimu 2018-19 Ziyech alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Uholanzi. Msimu huu hadi sasa amefunga mabao manane na kupiga pasi za mabao 21 kitu ambacho kinamfanya kuwa mfalme wa asisti kwa sasa barani Ulaya - kwa sababu idadi hiyo ni kubwa zaidi kuliko mchezaji yoyote Ulaya.

Soka la kimataifa

Ziyech alikuwa na uwezo wa kuchagua kuchezea timu ya taifa ya Uholanzi au Morocco. Akiwa kijana mdogo alichezea vikosi vya vijana vya Uholanzi chini ya miaka 19, 20 na 21, lakini Septemba 2015 aliamua kuichagua timu ya asili ya wazazi wake Morocco ambayo ndiyo anaichezea hadi sasa.

Staili ya uchezaji

Ziyech ni winga anayeweza kucheza kwenye pande zote mbili kulia na kushoto, huku ubora wake ukiwa kwenye kukokota mpira, kufunga, kupiga pasi ndefu, ufundi mwingi na uwezo mkubwa wa kupiga mipira iliyokufa.