Haijawahi kutokea ……

Saturday February 27 2021
luis miqusson pic
By Thobias Sebastian

KAMA kweli Simba ikipata mkwanja inaotaka kwa staa wao, Luis Jose Miquissone huenda ikaandika rekodi ya dau ambalo halijawahi kutokea kwenye usajili katika siku za hivi karibuni.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba kimethibitisha kwamba kiwango ambacho alionyesha Miquissone katika mechi ya Al Ahly kimewaibua matajiri wengi Afrika ambao wanamiliki timu mbalimbali na kutaka huduma ya mchezaji huyo.

Miongoni mwa timu ambazo zimeshaonyesha nia ya wazi wazi kwa Simba na kuulizia mkataba wa Miquissone ukoje ni Al Ahly, CD Belouizdad ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Sauzi.

luis miquison pic 2

“Ukiachana na timu hizo tatu ambazo zimeonyesha nia ya kumtaka mchezaji wetu na kuulizia upatikanaji wake pamoja na mkataba wake ulivyo kuna nyingine kutoka Misri, Morrocco, Algeria na Afrika Kusini,” alidokeza mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba.

“Lakini nataka nikwambie sisi kwenye vikao vya ndani tumekubaliana kwamba dau la chini kabisa kumuuza huyo mchezaji ni Dola 1 milioni (Sh2.3Bilioni)hicho ndio kigezo cha kwanza,” alisema.

Advertisement

“Jambo la mwisho wanatakiwa kumlipa mshahara kuanzia Dola 35,000(Sh81milioni) na isipungue Dola 28,000(Sh65milioni). Na kamati yetu ya usajili tumeshaanza kutafuta mbadala wa Miquissone kwani tunatambua kuanzia mwezi Juni kuna ofa nyingi tutapokea na hatutaweza kubaki nae.

“Tayari tumeanza kuwafuatilia wachezaji mbalimbali kwani tunatambua kuwa kama Miquissone atacheza katika kiwango kama cha wakati huu hatutaweza kubaki nae,”alisema kigogo huyo wa Simba ingawa jana Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez hakujibu alipoulizwa kuhusu nini kinaendelea kwa staa huyo.

Katika hatua nyingine, Ofisa habari wa Simba, Haji Manara alisema hao wachezaji ambao wanapata madili makubwa kwenda kucheza katika timu nyingine nao ni binadamu na wana mahitaji yao.

Manara alisema kama ikija ofa iliyoshiba ya Miquissone wanaweza kujikuta wanaikataa kwa kutaka kubaki na mchezaji wiki moja mbele anavunjika mguu na kuanza kuikumbuka ile pesa.

“Hakuna klabu yoyote ya mpira duniani nayo itakaa kuuza mchezaji kama kuna nyingine ambayo inaweza kuwapatia maslahi ambayo watakuwa wanahitaji.

“Kama kuna klabu imefika bei ambayo Simba itakuwa imeweka kwa ajili ya kumuuza Miquissone wakete hiyo pesa tutawachia mchezaji,” alisema Manara.

Miongoni mwa mauzo makubwa ya wachezaji ambayo Simba imewahi kufanya ni Mbwana Samatta Sh346milioni kwenda TP Mazembe na Sh692milioni Emanuel Okwi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia.

Advertisement