Gomes aridhishwa na akina Ajibu!

KOCHA wa Simba, Didier Gomes anasema ameridhika na viwango ambavyo walionyesha wachezaji wake ambao huwa hawatumiki mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.

Gomes anasema kikosi cha Simba kinawachezaji wote wazuri ila huwa anatoa nafasi ya kucheza kutokana na wapinzani wao walivyo, mahitaji ya mechi na viwango ambavyo wanaonyesha katika mazoezi.

"Mabadiliko ambayo yalifanyika katika mechi ya ASFC, dhidi ya African Lyon ni kutokana na baadhi ya wachezaji kutumika zaidi nikawapa muda wa kupumzika na kujiandaa kwa ajili ya michezo iliyokuwa mbele yetu," anasema.

"Kuna baadhi ya wachezaji wengine kama Luis Jose Miquissone mara baada ya kumaliza kucheza mechi na Al Ahly hakuwa sawa ilibidi waonane na Daktari pamoja na kupata muda wa kupumzika na matibabu," anasema.

"Nimevutiwa na vile ambavyo wamecheza na wameongeza ushindani ndani ya kikosi kama ambavyo nilikuwa nategemea kutoka kwao na kazi imebaki kwangu kuchagua ambao watakuwa wanafaa kutuwakilisha kulingana na mahitaji ya mechi," anasema Gomes.

Kikoisi cha Simba jana kilianza na kipa, Aishi Manula, Kennedy Juma, Gadiel Michael, Ibrahim Ame, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Rally Bwalya, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu na Parfect Chikwende.

Wachezaji waliopata nafasi ya kuanza katika kikosi hicho cha kwanza ambao huwa hawatumiki mara kwa mara katika kikosi cha kwanza ni, Gadiel, Ame, Nyoni, Kennedy, Kagere, Ajibu na Dilunga.