Gomes awajaza upepo Morrison, Kagere
ACHANA na matokeo ya mechi yao ya jana, unaambiwa Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amekuja na mbinu mpya mbili kuhakikisha kikosi chake kinapata matokeo mazuri katika michezo mfululizo ya kimashindano iliyokuwa mbele yao, akiwajaza upepo nyota wake Meddie Kagere, Bernard Morrison na wengine ili kutisha zaidi.
Mbinu ya kwanza ambayo Gomes amekuja nayo katika kikosi hicho cha Simba kabla ya kucheza mechi yoyote huwa anakaa na wachezaji wake katika chumba cha mkutano wakiwa katika kambi yao au kwenye eneo ambalo wamefikia kwa ajili ya mchezo.
Baada ya kukaa na wachezaji wake wote huwa anachukua kanda za video za timu wanayoenda kucheza nayo kisha wanaangalia ambavyo wanacheza kwa maana kushambulia, kukaba, ubora, madhaifu, mchezaji wao hatari na mambo mengine ya kiufundi.
Wakishamaliza kuangalia hizo video mbele yake huwa na ubao pamoja na makapteni hutumika kuwaelekeza wachezaji wake vya kwenda kufanya kwa maana kuzuia ubora wao, kushambulia kutokana na mapungufu ya wapinzani yalivyo pamoja na mambo mengine.
Gomes baada ya hapo kile kile ambacho wamekifanyia kazi kwa maneno wakiwa katika mkutano wao kutokana na video za wapinzani walivyo wanakwenda kuvifanyia kazi kwa vitendo wakiwa katika uwanja wao wa mazoezi.
Ukiachana na mbinu hiyo Gomes ameleta mbinu nyingine akiwa kambini amekuwa anaongea na kila mchezaji kutaka amueleza kila ambacho anahitaji kifanyike lakini kama kuna mapungufu pia dhidi yao ambayo anatakiwa yafanyiwe kazi huwa anawaeleza.
Miongoni mwa wachezaji ambao tayari ametenga muda na ameongea nao kila mmoja kwa nafasi yake ni Bernard Morrison na Meddie Kagere ambaye anashika nafasi ya pili katika ufungaji akiwa amefunga mabao saba.
Gomes alisema kutokana na ugeni wake katika timu ilikuwa lazima apate muda wa kutosha kuangalia video za mechi za timu pinzani ambavyo wanacheza ili kufahamu taarifa nyingi na akikutana nao asipate shida ya kukabiliana nao.
“Baada ya kuangalia hizo video za timu pinzani kama Dodoma Jiji, Namungo, Yanga, Azam na nyinginezo nyingi huwa nakaa tena na wachezaji wangu kuwaonyesha kile cha kwenda kukifanya na hatuishii hapo bali tunajiandaa pia katika mazoezi kama ambavyo tulielekezana,” alisema.
“Kweli nimekuwa naongea na kila mchezaji mmoja mmoja tukiwa wawili tu ili aweze kunieleza kile ambacho anakiona ndani ya timu, kama kuna shida yoyote.”