Morrison azidisha utamu Simba

Muktasari:
Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu, KMC imeifumua Namungo bila huruma kwa mabao 3-0.
Dodoma. Mabingwa wa soka nchini, Simba, wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji, wakati kiungo wake, Benard Morrison akitoa pasi ya bao na kufunga la ushindi kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini hapa.
Morrison aliifungia Simba bao la ushindi kipindi cha pili baada ya kutoa pasi ya bao la kwanza wakati, kipindi cha kwanza kikimalizika kwa sare ya 1-1.

Wakati Simba ikizidi kuisogelea Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, KMC ilitumia vizuri Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Namungo FC.
KMC imeanza kunufaika na usajili wao wa dirisha dogo baada ya Charles Ilanfya na Matheo Anthony waliosajiliwa sasa kuingia katika kitabu cha wafungaji.
Jijini Dodoma, ushindi wa Simba umeonekana kuwa na dalili nzuri kwa kocha mpya wa mabingwa hao watetezi, Didier Gomez, ambaye ndiyo mchezo wake wa kwanza kusimama kama kocha katika ligi.

Kocha huyo raia wa Ufaransa alisema ushindi huo una maana kubwa kutokana na kuhitaji kwake kusogea kileleni mwa msimamo unaoongozwa na Yanga.
“Lengo ni kusogea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, tupo nyuma ya Yanga kwa pointi sita na tunahitaji kufanya hivyo kwani ubingwa ndiyo kitu tunachokihitaji zaidi kwasasa.
“Tunautazama mchezo ujao sasa dhidi ya Azam FC, wana timu nzuri kutokana na nafasi waliyopo japo sijawahi kuwaona uwanjani, hivyo tunarudi kujiandaa kwa ajili ya pointi tatu nyingine,” alisema Gomez.
Kocha wa Dodoma Jiji, Mbwana Makatta aliwapongeza vijana wake kwa kucheza vizuri huku akisisitiza kuwa makosa madogo yalisababisha kupoteza mchezo huo muhimu.
Makatta alisema aliitazama Simba hasa baada ya vijana wake kuruhusu bao la kwanza hivyo kufanya mabadiliko aliyoamini yalikuwa na faida kubwa kwa dakika zilizobaki.
“Vijana walicheza vizuri lakini nilihisi kuna kitu kinakosekana kwa vijana wangu, ndiyo maana nilimtoa Steven Mganga na kumwingingiza Cleoface Mkandala na kila mtu ameona nini nilikuwa namaanisha.
“Lakini bado kulikuwa na makosa madogo wakati wa kutoa timu nyuma, kitu ambacho kilifanya tushambuliwe kwa kushitukizwa na kusabababisha bao la pili,” alisema Makata.
Katika mchezo huo, Simba ilianza kuandika bao la kwanza kupitia kwa mahsmbuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere, aliyetumia krosi ya Morrison kwa kona fupi.
Hilo linakuwa bao la nane kwa mshambuliaji huyo licha ya kucheza kwa dakika chache katika mechi za ligi msimu huu.
Baada ya bao hilo, kocha Makata wa Dodoma Jiji aliamua kumtoa Maganga na kumwingiza Mkandala, ambaye mguso wake wa kwanza ulitokana na mpira wa kona ya Dickson Ambundo.
Mkandala alikutana na mpira wa Ambundo akifunga bila kukabwa kama ilivyokuwa kwa Kagere alipoifungia Simba bao la kuongoza na kufanya matokeo kuwa 1-1 hadi mapumziko.
Kocha wa Simba, Gomez aliamua kumtoa Luis Miquessone na nafasi yake kuchukuliwa na Perfect Chikwenda kwa ajili ya kuongeza presha wakionyesha kuhitaji ushindi katika mchezo huo ulioshuhudiwa na wabunge wengi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pasi ya Chikwende iliyotokana na kuanzishwa mashambulizi na kiungo wa kimataifa wa Zambia, Larry Bwalya, ilikwenda vizuri kwa Morrison, ambaye bila ajizi alijitengenezea na kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Dodoma Jiji, Aaron Kalambo.
Bao hilo liliifanya Simba kutuliza presha na kurudi katika soka lao la kawaida huku wakijilinda zaidi, jambo lililomfanya poia kocha wao kumwingiza kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin.
Kipa wa Simba, Aishi Manula, alilazimika kufanya kazi ya ziada dakika ya mwisho ya nyongeza, wakati mpira wa adhabu ndogo uliounganishwa kwa kichwa langoni mwake ulipotaka kuisawazishia Dodoma Jiji.
IMEANDIKWA NA Matereka Jalilu