Gomes ataja sifa 4 kikosi cha kwanza

Muktasari:

KOCHA wa Simba, Dider Gomes amesema kwenye kikosi chake hakuna mwenye namba ya kudumu,ili upate nafasi hiyo ni lazima uwe na sifa nne.

KOCHA wa Simba, Dider Gomes amesema kwenye kikosi chake hakuna mwenye namba ya kudumu,ili upate nafasi hiyo ni lazima uwe na sifa nne.

Gomes alizitaja sifa hizo ni nidhamu, umakini, kusimamia misingi ya soka na kufanya kazi kwa bidii na malengo kila sekunde pamoja na kujitunza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gomes alisema ili ashawishike na kumwamini kumpa mchezaji namba ni lazima mwenyewe ajipime kwa sifa hizo.

“Hakuna mchezaji aliyesajiliwa na uongozi wa Simba atakosa nafasi ya kucheza chini yangu kila mmoja atacheza kikubwa ni kuzingatia kile ninachokifundisha sambamba na kujituma,” alisema.

“Nidhamu ni kitu muhimu sana kwangu na huwa ni mkali sana ninapomuona mchezaji anaonyesha utovu wa nidhamu na mara nyingi hua siwapi nafasi wachezaji wa namna hiyo.”

Alisema timu yake ina nyota wengi wenye uwezo wa kucheza lakini wamekuwa wakikosa nafasi kutokana na kushindwa kufuata kile anachokihitaji kama kujituma na kutambua nini wanatakiwa kukifanya ili timu iwe bora.

“Siwezi kuchezesha nyota wote waliosajiliwa kutokana na ubora wao hapana hilo haliwezekani kwenye maisha ya soka wachezaji ni 11 tu uwanjani ili uweze kuwa miongoni mwa nyota hao unatakiwa kufuata misingi ya soka kujituma sana ili kunishawishi na kuonyesha utofauti na wengine,” alisema Gomes

Ibrahim Ame ambaye yupo kwa mkopo Mtibwa Sugar akitokea Simba, alisema: “Gomes ni kocha ambaye amekuwa akisisitiza sana nidhamu kwa wachezaji nje na ndani ya uwanja. Anapoona mchezaji amekosa nidhamu huwa anamuita na kuzungumza naye kwa ni ya kumrekebisha.

“Nimeshuhudia baadhi ya wachezaji wengine kukosa nafasi kwa utovu wa nidhamu na amekuwa akiwaweka nje kama fundisha, sijawahi kupata tatizo lolote la kinidhamu, nilikosa namba kwa sababu ya ushindani tu.”

Ame ambaye alikuwa anakalishwa benchi na Paschal Wawa, Joash Onyango na Kennedy Juma.