Gerrard afunguka ishu ya familia

LONDON, ENGLAND. STEVEN Gerrard amekiri mkewe, mrembo Alex anataka aachane na mambo ya ukocha ili kuepuka presha na kwenda kutulizana na familia yake.
Kiungo huyo wa zamani wa Liverpool na England, Gerrard, 40, kwa sasa ni kocha wa Rangers akichukua mikoba hiyo zaidi ya miaka miwili iliyopita na kutengeneza timu yenye uwezo wa kubeba ubingwa wa Scotland.
Gerrard, ambaye alipata mafanikio makubwa akiwa mchezaji huko Liverpool, amekubaliana na kila kitu kuhusu ajira yake mpya ya ukocha na kusema presha ni kubwa.
Lakini, Gerrard alisema anafahamu wazi familia yake inakosa muda wa kutosha wa kuwa pamoja.
“Kuna nyakati hizo zinamiliki maisha yake na huwezi kuzizuia. Hivyo ndivyo mambo yalivyo.
“Lakini, utafika wakati katika maisha yangu itabidi niachane na kila kitu kwa ajili ya familia yangu na mimi mwenyewe. Kuachana na kila kitu na kuishi maisha ya amani.
“Kwa sasa bado nina nguvu ya kutosha. Bado naweza kuwasaidia wachezaji. Bado nina nafasi ya kufanya vizuri zaidi. Kwa mke wangu, Alex na watoto wetu, utafika wakati nitakuwa nao kwa asilimia 100. Ni lini, nani anajua? Alex atakwambia iwe kesho,” alisema Gerrard baba wa watoto wanne.
Gerrard na Alex walifunga ndoa mwaka 2007 na amekuwa naye kwa muda wote kwenye nyakati nzuri na mbaya akiwa Liverpool na misimu yake miwili huko LA Galaxy ya Marekani.