Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gamondi aanza na rekodi mpya

WAKATI makocha wengine wakikuna vichwa jinsi ya kuwatumia wachezaji, hali ni tofauti kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi kwani licha ya kukabidhiwa kikosi msimu huu tayari asilimia 99 ya nyota wote 26 wamecheza michuano mbalimbali huku Dickson Job na Kouassi Yao wakifunika.

Yanga imecheza mechi tisa kwenye mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja na mchezo mmoja wa wiki ya Mwananchi ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya kutambulisha kikosi cha msimu huu.

Katika mechi tisa, timu hiyo imefunga mabao 23 ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja ambapo ilianza dhidi ya Kaizer Chiefs na kushinda bao 1-0, dhidi ya Azam FC kwenye Ngao ya Jamii ikashinda 2-0, Ligi ya Mabingwa hatua ya awali na Asas FC ilishinda mabao 2-0 na ule wa marudiano ikashinda 5-1.

Mechi za ligi ilianza na KMC ikaibuka na ushindi wa mabao 5-0, JKT Tanzania 5-0 na dhidi ya Namungo bao 1-0 huku ikiifunga Al Merreikh mabao 2-0.

Ushindi wa Yanga katika mechi zote hizo umechangiwa na kikosi chote kutokana na kocha Gamondi kutoa nafasi kwa kila mchezaji, huku kipa Abuutwalib Mshery akiwa ni pekee aliyekosa nafasi ya kucheza kutokana na kutoka kuuguza majeraha.

Wakati mastaa hao wakihusika kasoro Mshery, kuna baadhi ya wachezaji licha ya kupata nafasi ya kucheza kwenye Wiki ya Mwananchi, Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa, wapo waliokosa nafasi ya kucheza mechi za ligi ambao kati ya 26 ni watatu tu.

Yanga tayari imecheza mechi tatu za ligi ikikusanya pointi tisa na mabao 11, huku nyavu zake zikiwa hazijatikishwa hata mara moja na mastaa ambao hawajahusika kwenye ushindi huo ni Gift Fredy, Mahlatsi Makudubela ‘Scudu’, Chrispin Ngushi na Kibwana Shomari ambaye alikuwa panga pangua kikosini msimu uliopita chini ya Nasreddine Nabi na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Wakati mastaa hao wakikosa nafasi mabeki Job na Yao wanaonekana kufunika zaidi kutokana na kutumika kwa dakika nyingi zaidi ya wengine huku nahodha Bakari Mwanyeto na kiungo Jonas Mkude wakitumika kwa dakika chache zaidi kwenye ligi wakicheza dakika saba katika mechi moja kati ya tatu.

Yao na Job kwenye mechi tatu za ligi wametumika kwa dakika 270 baada ya kucheza mechi zote kwa dakika 90 wakati wawili hao wakicheza dakika hizo, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ amefuata kwa kucheza dakika 264, Khalid Aucho 253, Stephane Aziz Ki 246, Keneddy Musonda 232, Mudathir Yahya 203, Maxi Nzengeli 197, Dickson Kibabage 185, Djigui Diarra 180, Pacôme Zouzoua 157, Jesus Moloko 102, Clement Mzize 98, Metacha Mnata 90, Konkoni 85, Joyce Lomalisa 59, Zawadi Mauya 28 na Farid Mussa 26.

Mwanaspoti lilizungumza na Gamondi ambaye alikiri kikosi chake kipo fiti na wachezaji wengi wana uwezo sawa ndio maana amekuwa akitoa nafasi kwa mastaa wote.

“Nafurahi kufanya kazi na Yanga ina wachezaji wengi wazuri na wote wana uchu wa mafanikio hiyo ndio inaweza kuwa siri ya matokeo mazuri ambayo tumekuwa tukiyapata ndani ya uwanja;

“Hatuna mchezaji tegemezi kila mchezaji anatumika kutokana na ushawishi wake mazoezini, kuhusu uwezo kwa asilimia kubwa wote wana uwezo sawa kinachotofautisha ni aina ya uchezaji na kila mmoja anatumika kutokana na aina ya mpinzani tunayekutana naye.”alisema Gamondi.