Fury vs Dillian Whyte rekodi tisa zisubiriwa kuvunjwa

Muktasari:
- Pambano la kesho litakuwa la kwanza mwaka huu kwa Fury bondia namba moja wa dunia wa uzani wa juu ambaye kama atapoteza, itakuwa ni anguko kubwa kwake tofauti na mpinzani wake ambaye hayupo kwenye renki ya dunia.
Wakati mashabiki wa ndondi duniani wakisubiri kuona kama Dillian Whyte atapindua meza mbele ya mbabe wa dunia wa uzani wa juu, Tyson Fury rekodi tisa zinasubiriwa kuvunjwa kwenye pambano hilo la kesho
Mabondia hao watazichapa kwenye uwanja wa Wembley jijini London Uingereza, Fury akicheza nyumbani kutetea ubingwa wa dunia wa kamisheni ya ngumi za kulipwa (WBC) ambao alimvua Deontay Wlider mwaka 2020 alipomchapa kwa Technical Knock Out (TKO) raundi saba na kuutetea mwaka jana alipomchapa kwa Knock Out (KO) ya raundi ya 11.
Pambano la kesho litakuwa la kwanza mwaka huu kwa Fury ambaye kama atapoteza, itakuwa ni anguko kubwa kwake tofauti na mpinzani wake ambaye hayupo kwenye renki.
Whyte kwenye rekodi za mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) ameeondolewa na kuwa 'inactive' baada ya kutocheza kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu Machi 27 mwaka jana alipomchapa Alexander Povetkin kwa TKO na kuwa bingwa wa WBC Interm.
Kwa mujibu wa Boxrec, bondia ambaye hajapigana kwa mwaka mmoja anondolewa kwenye renki, hivyo pambano la kesho litamrejesha upya na kama atashinda, litampandisha mara dufu kwenye ubora tofauti na Fury ambaye akishinda ataongeza pointi kadhaa na endapo atapigwa ataporomoka na kuandika rekodi ya kwanza ya kipigo.
Bondia huyo hajawahi kupoteza pambano kati ya 32 aliyocheza, ameshinda mara 31 na kutoka sare na Wilder tangu alipoingia kwenye ngumi za kulipwa.
Whyte yeye ana historia ya kupigwa mara mbili, zote kwa KO ikiwamo ya Anthony Joshua mwaka 2015 na Povetkin mwaka 2020 kabla ya kulipa kisasi mwaka 2021 kwa TKO na hakuwahi kurudi ulingoni hadi alipofutwa kwenye renki.
Rekodi nyingine inayosubirwa kuvunjwa kesho ni ya Nick Ball anayecheza pambano la utangulizi dhidi ya Isaac Lowe, kama Ball atapigwa ataandika historiaya kupigwa kwa mara ya kwanza kwenye ngumi za kulipwa ambapo amekwishapigana mapambano 14 na kushinda yote.
Mpinzani wake ni bondia mzoefu aliyepanda ulingoni mara 25 na kushinda mapambano 21, amepigwa mara moja na kutoka sare mapambano matatu.
mabondia hao watawania ubingwa wa WBC Silver kwenye uzani wa Feather, pambano ambalo litakuwa la mwisho la utangulizi kabla ya Furry na Whyte kupanda ulingoni.
Rekodi nyingine ni ile ya Ekow Essuman ambaye pia hajawahi kupigwa kwenye mapambano 16 atakayemkabiri Darren Tetley kuwania ubingwa wa Commonwealth (British Empire) kwenye uzani wa welter na ubingwa wa International Boxing Federation European.
Wengine ambao rekodi zao za kutopigwa zinasubiriwa kuvunjwa ni David Adeleye atakayezichapa na Chris Healey, Tommy Fury dhidi ya Daniel Bocianski na bondia chipukizi, Kurt Walker atakayecheza pambano lake la pili kesho dhidi ya mkongwe mwenye rekodi ya kupigwa mara 31, kushinda mara tatu na kutoka sare mara mbili, Stefan Nicolae.
Rekodi nyingine ni ya Karol Itauma atakayezichapa na Michal Ciach aliyeshinda mara mbili tu kati ya mapambano yake 13 na chipukizi, Royston Barney-Smith atakayezichapa pambano lake la pili na Constantin Radoi ambaye hajawahi kushinda kwenye mapambano 10 aliyopigana.