Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fei Toto aiwahi Dodoma Jiji

FEI Pict

Muktasari:

  • Azam imesalia mechi tatu dhidi ya Dodoma jiji iliyopangwa kupigwa Mei 13, kabla ya kuvaana na Tabora United na kumalizana na Fountain Gate, huku timu hiyo ikipambana kumaliza katika nafasi ya tatu ili ikate tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

AZAM FC inaendelea kujifua kwa ajili ya mechi tatu za kumalizia msimu wa Ligi Kuu, lakini taarifa njema ni kwamba kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyekosekana katika mechi tatu zilizopita kutokana na kuwa majeruhi amerejea uwanjani na kuiwahi Dodoma Jiji.

Azam imesalia mechi tatu dhidi ya Dodoma jiji iliyopangwa kupigwa Mei 13, kabla ya kuvaana na Tabora United na kumalizana na Fountain Gate, huku timu hiyo ikipambana kumaliza katika nafasi ya tatu ili ikate tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Azam iliyong’oka mapema katika mbio za ubingwa, huku ikitolewa pia katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), hiyo ndio nafasi pekee ya kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi, ikichuana na Singida Black Stars iliyopo nafasi ya nne na iliyopo nusu fainali ya Kombe la FA ikisubiri kucheza na Simba.

Ujio wa Fei Toto umelipa faraja benchi la ufundi la timu hiyo, lililomkosa katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar iliyoshinda mabao 4-2 mjini Bukoba, kisha kucheza mechi mbili za Kombe la Mapinduzi, ikishinda 1-0 katika robo fainali dhidi ya KMKM na kupasuka 2-1 kwa  JKU.

Fei amerejea wakati Azam ikijiandaa kukabiliana na Dodoma Jiji, huku kocha wa kikosi hicho, Rachid Taoussi, amesema uwepo wa staa huyo unaongeza nguvu katika timu hiyo kwa pambano hilo litakalopigwa Mei 13, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Taoussi alisema kurejea kwa Fei kutaongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ambayo kwa mechi za hivi karibuni imeonekana butu na kuishia kutegemea juhudi binafsi za nahodha na beki wa kulia, Lusajo Mwaikenda kuifungia mabao timu hiyo.

“Ni wazi kumkosa Fei kikosini sio kazi rahisi, kila mtu anafahamu ubora na uimara alionao, hivyo kurejea kwake kunanipa matumaini makubwa. Nafurahia kurejea mazoezini kwanza, ambako tunajinoa kwa ajili ya mchezo ujao, akifanya vizuri huku, basi atasaidia kuipa nguvu safu ya ushambuliaji,” alisema Taoussi na kuongeza;

“Kweli tumesalia na mechi chache mkononi, ila haimaniishi tulegeze kamba bali tunatakiwa kukaza zaidi, kwani mipango ni ile ile, kumaliza kwa ushindi. Kila mpinzani anayekuja kwetu sasa anataka kujiongezea alama ili kuwa salama zaidi na sisi pia hatujaridhika, ndio maana naongea na wachezaji wangu kuwa, kushinda ni lazima.”

Fei Toto ndiye mchezaji anayeongoza kwa asisti nyingi msimu huu akiwa nazo 13, akiwa pia amefunga mabao manne, huku msimu uliopita uliokuwa wa kwanza kwake klabuni Azam alikojiunga akitokea kwa mabingwa wa kihistoria, Yanga, alifunga mabao 19 na kutoa asisti saba. Alimaliza wa pili nyuma ya mshindi wa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu, Stephane Aziz Ki wa Yanga (21).

Hata hivyo, Azam imesalia na mechi tatu kumaliza ligi, huku ikiwa na rekodi ya kuzichapa timu mbili raundi ya kwanza ambazo ni Dodoma Jiji 1-3 na Fountain Gate 2-0, huku ikipigwa ugenini na Tabora United 2-1.