Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Faili la Jonathan Sowah latua kwa MO

SOWAH Pict

Muktasari:

  • Nyota huyo wa kimataifa kutoka Ghana, awali amekuwa akihusishwa na Yanga iliyoelezwa ilijifungia naye jijini Dar es Salaam Aprili mwaka huu ili kuwekana sawa.

KABLA hata dirisha la usajili halijatangazwa kufunguliwa, mabosi wa klabu kubwa za soka nchini wameanza kazi kimyakimya kusaka nyota wapya kwa msimu ujao, huku faili ya straika wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah likitua kwa bilionea wa Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji.

Nyota huyo wa kimataifa kutoka Ghana, awali amekuwa akihusishwa na Yanga iliyoelezwa ilijifungia naye jijini Dar es Salaam Aprili mwaka huu ili kuwekana sawa, huku Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ikitajwa kummezea mate baada ya kocha wa timu hiyo Nasreddine Nabi kuibuka nchini hivi karibuni.

Taarifa mpya ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni kwamba kocha wa Simba, Fadlu Davids amewasilisha jina la straika huyo mezani kwa MO Dewji akitaka asajiliwe kama sehemu ya mpango wa maboresho ya kikosi kuelekea msimu ujao.

Hatua hiyo imeashiria mwanzo wa mbio kali za kusaka saini ya Sowah, ambaye amedhihirisha kuwa si mshambuliaji wa kawaida kutokana na uwezo wake wa kutumia nguvu, akili na nafasi kwa ufasaha mkubwa, akifunga mabao 11 kupitia mechi 12 za Ligi Kuu mbali na mabao mengine ya Kombe la FA.

Inaelezwa Fadlu yupo mbioni kusaka mshambuliaji atakayetoa changamoto ya nguvu kwa waliopo sasa kikosini yaani Leonel Ateba na Steven Mukwala, ambao licha ya kufunga mabao 24 kati yao msimu huu kwenye ligi, bado wameonekana kuwa na upungufu katika maeneo fulani ya kiufundi.

Kwa Fadlu, Sowah ni zaidi ya mfungaji ni mchezaji anayewasukuma mabeki kuwa kwenye tahadhari muda wote, jambo ambalo ni la muhimu sana katika mfumo wake wa uchezaji unaopendelea presha ya juu na mpira wa kushambulia kwa kasi.

Ujio wa Sowah katikati ya msimu kutoka Al-Nasr Benghazi ya Libya ulionekana kwa wengi kama dili la kawaida kwa klabu inayojijenga kama Singida BS, lakini ndani ya muda mfupi ameibadilisha klabu hiyo na kuifanya kuwa tishio, huku akiifungia mabao muhimu katika mechi kubwa.

Kilichoongeza ladha ya habari hizi ni mazungumzo ya faragha kati ya Sowah na Fadlu kabla ya mechi ya nusu fainali ya Shirikisho, jambo lililofichua kuwa tayari kuna ishara ya nia ya Simba kuanza mazungumzo ya ana kwa ana na mchezaji huyo ili kutua Msimbazi.

Lakini kama ilivyo kawaida ya usajili wa nyota wanaong’ara kwenye soka la Afrika Mashariki, vita si ya klabu moja au mbili tu. Yanga mahasimu wa jadi wa Simba, nao wameripotiwa kumweka Sowah kwenye rada, hasa baada ya kuibuka kwa taarifa za mshambuliaji, Clement Mzize, huenda akavuka mipaka ya Tanzania kuelekea Afrika Kaskazini au Ulaya.


SIMBA YAONJA MAKALI

Katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Bara iliyofanyika Mei 28 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, Simba ililazimika kujitahidi mno kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida BS.

Hata hivyo, kilichobaki vichwani mwa mashabiki wengi wa Simba si bao la ushindi, bali ni namna ambayo Sowah aliwapa wakati mgumu mabeki wao huku akiangushwa mara mbili ndani ya boksi na kulamikia penalti ambazo hakupewa.

Kasi yake, uwezo wake wa kumiliki mpira akiwa mgongoni kwa beki, na ujasiri wa kupenya hadi kwenye boksi kwa kasi, vilimfanya kuwa tishio.

Baada ya siku tatu, kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA iliyochezwa Manyara, Sowah aliendelea kuwasumbua mabeki wa Simba kwa kiwango kikubwa zaidi, na safari hii akaweka jina lake kwenye orodha ya wafungaji, akiiwezesha Singida kupata ushindi wa kihistoria wa mabao 3-1.


WASIKIE SINGIDA BS

Mtendaji Mkuu wa Singida BS, Jonathan Kasano alisema: “Sisi hatuzuii mchezaji kupata maendeleo zaidi. Hata hivyo, kwa mchezaji kama Sowah ambaye ameweka historia kubwa ndani ya muda mfupi, tunahitaji mazungumzo ya kina. Klabu yoyote inayotaka huduma yake lazima ije na ofa ya  yenye mashiko.”

Kwa sasa, hatua iko mezani kwa Mo Dewji. Kama ataridhia ombi la Fadlu na kuidhinisha bajeti ya kumvuta Sowah Msimbazi, basi Simba inaweza kuizidi kete Yanga na Kaizer Chiefs kwenye mbio hizi.

Hata hivyo, ikiwa Simba watasita, kuna uwezekano mkubwa mshambuliaji huyo akaelekea moja kwa moja kwa wapinzani wao au Afrika Kusini, kwani Kaizer Chiefs, nayo imeingia kwenye orodha ya timu zinazomfuatilia Sowah kwa karibu.

Kocha Nasreddine Nabi, ambaye aliwahi kufundisha Yanga, alihudhuria mechi ya kiporo kati ya Simba na Singida akiwa sambamba na skauti wa klabu hiyo. Vyanzo vinaeleza kuwa aliridhishwa na kile alichokiona, na tayari ametoa ripoti ya awali kuhusiana na uwezekano wa kumsajili mshambuliaji huyo.


FADLU ANAVYOMTAZAMA

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, Fadlu amevutiwa zaidi na aina ya uchezaji wa Sowah ambayo inakamilisha mapungufu ya safu yake ya mbele.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, anayependelea kutumia mfumo wa mshambuliaji mmoja anayeweza kutoa presha kwa mabeki, ameona ndani ya Sowah kila kitu anachokitafuta nguvu, kasi, uelewa wa mpira na njaa ya mabao.

Hili linakuja wakati ambao Leonel Ateba ameonyesha kushindwa kutumia nafasi anazopata, licha ya kuaminiwa sana na kocha.

Katika mahojiano na baadhi ya watu wa karibu na benchi la ufundi la Simba, imethibitishwa kuwa Fadlu anataka mshambuliaji wa kiwango cha juu atakayeweza kuhimili mashindano ya ndani na ya kimataifa, huku akitoa ushindani wa kweli kwa washambuliaji waliopo.

Sowah, ambaye ameifungia Singida mabao 11 katika mechi chache, ameonekana kuwa suluhisho linalowezekana.