Edna, Mapunda wamkuna bosi Biashara United

RAIS wa timu ya Biashara United Mara kutoka Musoma, Revocatus Gabriel ameonekana kuridhishwa na utendaji kazi wa benchi la ufundi la timu hiyo kutokana na namna ambavyo wameimarisha kikosi.
Benchi la ufundi la Biashara linaongozwa na Amani Josiah ambaye aliipandisha Ligi Kuu mwaka 2018, akisaidiwa na kocha wa zamani wa timu ya Yanga Princess, Edna Lema, pia kipa wa zamani wa Yanga na Simba, Ivo Mapunda kama kocha wa makipa pamoja na wengine.
Rais huyo juzi alishuhudia timu yake ikianza kwa sare ugenini katika Ligi ngumu ya Championship dhidi ya Mbuni FC jijini Arusha baada ya kufungana bao 1-1, huku wanajeshi wa mpakani wakitandaza soka safi na kuwashangaza machalii na alisema licha ya kwamba ndio ligi imeanza lakini ana imani kubwa na benchi lake la ufundi.
Alisema moja kati ya jambo ambalo lilikuwa linawaumiza kichwa ni namna gani watakuwa na benchi nzuri la ufundi ambayo inaeleweka ndiyo maana waliamua kuwatafuta watu wenye uzoefu na ligi ngumu ili kuweza kupambana na kuipandisha timu daraja ambayo ndio malengo yao.
“Sisi kama uongozi tumeshafanya kazi yetu na tumewapa malengo yetu kwa hiyo inabidi wahakikishe wanaendelea kupambana zaidi ili timu ipande daraja,” alisema Revocatus.
Aliongeza msimu uliopita changamoto ambayo iliwanyima kupanda Ligi Kuu ni kufungiwa usajili ambayo iliwalazimu kuwatumia wachezaji vijana lakini baada ya kufunguliwa wamejitahidi kuhakikisha wanafanya usajili ulio bora zaidi.
Kwa upande wake kocha msaidizi wa timu hiyo, Edna Lema alisema licha ya kuwa timu yake ni mpya lakini wachezaji kila mmoja kwa nafasi yake anapambana ili kuhakikisha wanapata matokeo na kuendelea kupambania malengo yao.
“Bado tunatengeneza timu ambayo inaweza kufanya vizuri kwa sababu ndio mwanzo wa ligi, kwa sasa tunajipanga na mchezo ujao dhidi ya TMA Stars”.
Biashara ambayo ilishuka daraja mwaka 2022, kwa msimu huu imefanya mabadiliko makubwa pia kwa upande wa wachezaji kwa kuwasajili nyota kadhaa akiwemo kiungo Mganda, Boban Zirintusa aliyetoka Express.
Wengine ni kipa David Kisu, Cyprian Kipenye, Malulu Masunga, Hebert Lukindo pamoja na wengine wengi.