Dube aishi kifalme Dar, atengewa Sh1 bilioni

LUGHA rahisi unayoweza kutumia ni kwamba Prince Dube anaishi kama mfalme ndani ya ardhi ya Jiji la Dar es Salaam. Pengine hakuwahi kufikiria kwenye maisha yake ya soka angekumbana na kinachoendelea kwenye maisha ya sasa.

Staa huyo alivunja mkataba na Azam hivi karibuni huku klabu hiyo ikimtaka kulipa Dola 300,000 zaidi ya Sh700 milioni ingawa yeye alitaka kuwalipa Dola 200,000 ambazo ni takriban Sh510 milioni na ushee wakamgomea.

Straika huyo anahusishwa na klabu nne ambazo ni Simba, Ihefu, Al Hilal ya Sudan na Highlanders ya Zimbabwe. Lakini Mwanaspoti linajua kuna vigogo wa Yanga wameingilia dili hilo kimyakimya na wameshamseti mchezaji huyo akaingia laini na ameshawaelewa ndio maana mambo mengine yanaenda kimyakimya.

Habari zinasema kwamba licha ya Simba na Al Hilal kupeleka ofa zilizowavutia Azam, lakini kuna watu wa karibu na Yanga ambao ndio waliomuwekea mchezaji huyo ulinzi mkali wa mabaunsa watatu ambao baadhi walionekana nae Kwa Mkapa alivyokuja kucheki mechi ya Yanga na Azam. 

Si Simba wala Hilal ambao wameshapata nafasi ya kuonana uso kwa uso na mchezaji huyo mpaka sasa na hawajui anapoishi Jijini Dar es Salaam kwani alisharudisha kila kitu cha Azam ambao sasa wanasubiri chao kiingie kwenye akaunti kuvunja mkataba unaomalizika 2026.

Mwanaspoti limeambiwa kwamba mabaunsa hao wako watatu na ndio wanaoratibu ratiba zake za siku kwasasa na haruhusiwi kufanya chochote bila wao kujua na wanalinda makazi yake saa 24 kwa kubadilishana ikiwa ni maelekezo maalum ya vigogo hao wanaoisapoti Yanga ambayo mpaka sasa haijajitokeza hadharani wala kupeleka ofa yoyote Chamazi.

Habari zinasema kwamba Yanga wamemwekea ulinzi huo siyo kwa kuihofia Azam, bali hawataki Simba ipate upenyo wowote wa kumshawishi mchezaji huyo ambaye hivi karibuni aliweka wazi kwa marafiki zake wa karibu kwamba hatacheza Msimbazi wala Hilal kwani akili yake iko Jangwani.

Habari zinasema kwamba mbali na ulinzi huo, mchezaji huyo raia wa Zimbabwe amepewa gari ya kisasa aina ya Subaru-Forester ambayo kwa makadirio ya kawaida thamani yake ni Sh28milioni pamoja na dreva ambaye ni Yanga kindakindaki.

Pia Dube ameahidiwa mkataba mnono Jangwani wa miaka miwili ambao huenda ukaigharimu klabu hiyo zaidi ya Sh1Bilioni ukijumlisha dau la Azam Sh 700 milioni na lake ambalo halitapungua Sh500 milioni.


Lakini kwenye makazi mapya ya Dube ambayo ni maeneo Masaki amewekewa thamani mpya za ndani zinazogharimu Sh30Milioni inasemekana zimetoka kwenye duka la mmoja wa wadhamini wa timu hiyo.

Yanga ndio klabu pekee kwenye miaka ya hivi karibuni ambayo imenyakua wachezaji wakubwa Azam wakiwa na mikataba ambapo awali iliwachukua Sureboy na Gadiel Michael.

Nyota huyo hajacheza mechi ya Azam FC tangu Februari 19 alipoingia kipindi cha pili dhidi ya Tabora United. Msimu huu Dube amecheza dakika 734 Azam FC.

Dakika hizo alizocheza ni katika mechi 12, huku akikosa mechi saba mpaka anaondoka.

Hivi karibuni mastaa wa zamani wa Yanga walielezea umuhimu wa Dube kutua katika kikosi hicho.

Sekilojo Chambua ambaye ni kiungo wa zamani wa Yanga aliyekuwa tishio akicheza nafasi kama ya Dube alisema Mzimbabwe huyo anaweza kushambulia akitokea pembeni kwa maana ya kucheza kama kiungo mshambuliaji wa kulia, kushoto lakini pia anacheza kama mshambuliaji wa mwisho au namba 10. “Dube kucheza Yanga? Yule anacheza kabisa sijajua litamalizikaje hili sakata, lakini kwangu binafsi naona kabisa nafasi yake kwenye kikosi chetu Yanga ipo,” alisema Chambua.

“Dude anaweza kushambulia kutoka pembeni maeneo yote mawili lakini hata akicheza pale kwa Musonda (Kennedy) au hata kama timu itaamua kucheza na mshambuliaji mmoja anaweza, anaweza kufunga na hata kupiga mashuti.

“Ni mchezaji mwenye bidii kubwa uwanjani, kasi, akicheza hata kwenye uso wa goli anaweza kuwa na ufanisi mzuri, unajua kuna wakati unaweza kuja kwenye timu bora kama Yanga akaweza kung’aa zaidi kushinda alipokuwa Azam,”alisisitiza.

Naye Abeid Mziba ‘Tekelo’ alisema; “Dube anaweza kushambulia akitokea pembeni na uzuri atakuja kujiunga na timu iliyokamilika tofauti na huko alikokuwa.”

“Wasiwasi wangu ni rekodi yake ya kuwa majeruhi mara kwa mara lakini ukiacha hilo Dube kama yuko sawasawa anaweza kuja kuongeza kitu kikubwa, hii iwe ameanza kikosi cha kwanza au hata akiingia kwa mabadiliko,”alisema.

Wanachomaanisha mastaa hao ni kwamba kikosi kimoja Yanga inaweza kupangwa hivi; Diarra, Yao, Bacca, Job, Lomalisa, Mudathir, Aucho,Pacome, Aziz, Maxi na Dube. 

Lakini inamaanisha ujio wa Dube unaweza kula jina la staa mmoja wa kigeni ambaye hana namba kwenye kikosi cha kwanza msimu huu kama alivyo Gift Fred wa Uganda.

Lakini Dube mwenyewe hivikaribuni alipoulizwa kuhusiana na sakata lake alisema: “Kuna mambo mengi hamuyajui wakati ukifika mtayajua, kwa sasa niacheni kwanza nitafakari.”