Dodoma Jiji noma, vinatoka vyuma zinaingia mashine

WAKATI wachezaji Dickson Ambundo na Aaron Kalambo wakiachana na Dodoma Jiji, timu hiyo ipo kwenye mawindo ya kunasa wachezaji wapya ambao wataziba nafasi za nyota hao akiwemo mshambuliaji Danny Lyanga wa JKT Tanzania.
Ambundo tayari ameshaanza kuichezea Yanga kwenye mashindano ya Kagame yanayoendelea jijini Dar es Salaam wakati Kalambo, kwa upande wake, anasubiri tu msimu uanze ili aanze maisha yake mapya akiwa na timu yake ya zamani, Tanzania Prisons.
Katibu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson aliweka wazi kuwa wapo mbioni kufanya usajili wa wachezaji maeneo manne akiwemo kipa, mabeki, viungo na washambuliaji.
Licha ya kwamba hakuweka wazi majina ya wachezaji wanaowafukuzia, lakini habari za ndani zinasema kuwa muda wowote wanaweza kumsainisha kipa aliyetemwa na Polisi Tanzania Mohammed Yusuph.
Mbali na kipa huyo, kipa mwingine ambaye anatajwa kama chaguo lingine la kuziba nafasi ya Kalambo, ni Ramadhan Kabwili wa Yanga, ambaye kama mambo yatakwenda ipasavyo, anaweza kujiunga kwa mkopo ndani ya kiksoi cha Dodoma Jiji msimu uajo.
Kwenye eneo la kiungo, jina la Meshack Abraham wa Gwambina, lipo kwenye rada za timu hiyo, baada ya timu yake kushuka daraja, jambo ambalo linamlazimu kiungo huyo matata kuwa tayari kusaini timu yoyote itakayomhitaji wakati kwenye ushambuliaji Dodoma Jiji inasaka saini za Lyanga na Vitalis Mayanga aliyetemwa na Kagera Sugar.