Dilunga aibeba Simba ikishinda kwa penalti dhidi ya Stand United

Muktasari:
Kiungo Dilunga ameibuka shujaa wa Simba baada ya kufunga penalti ya mwisho pia ikiwa ni penalti yake ya pili katika mchezo huo.
Dar es Salaam. Kiungo Hassan Dilunga ameiongoza Simba kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (ASFC) kwa kuichapa Stand United kwa penalti 3-2 baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare 1-1 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Kiungo Dilunga ameibuka shujaa wa Simba baada ya kufunga penalti ya mwisho pia ikiwa ni penalti yake ya pili katika mchezo huo.
Dilunga alikwenda kupiga penalti ya tano na kupiga shuti la chini na kumwacha kipa wa Stand United akiwa hajui la kufanya.
“Penalti haina ufundi ila unapojiamini unapokwenda kupiga inakuwa rahisi kwao kufunga,” alisema Dilunga.
Dilunga alisema kukosa penalti kwa Meddi Kagere ni kawaida kwa mchezaji bora kupoteza hivyo siyo ya tatizo.
“Tumeona Messi, Ronaldo wote wakikosa penalti hivyo hakuna ajabu kwa Kagere kukosa jambo la msingi naamini kuna kitu amejifunza na siku nyingine atafanya vizuri,” alisema Dilunga.
Mbali ya Dilunga wengine waliopata penalti kwa Simba ni Clatous Chama, na Deo Kanda wakati Kagere na Ibrahimu Ajibu wakikosa penalti zao.
Upande wa Stand United waliopata penalti ni Faki Juma, Brown Raphael huku Miraji Salehe, Majid Kimbonidile na Maulid Fadhiri wakikosa penalti zao
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Dilunga katika dakika 51, baada ya beki wa Stand United kushika mpira wakati akijaribu kuokoa.
Wenyeji Stand United walisawazisha bao hilo katika dakika 67 kupitia Miraji Salehe akiunganisha krosi ya Maulid Fadhili aliyemtoka beki wa Simba.
Katika michezo mingine ya raundi hiyo Mbeya City imeaga mashindano baada ya kufungwa na Namungo kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati Ndanda FC ikiwa nyumbani uwanja Nangwanda Sijaona Mtwara imeichapa Kitayosa FC kwa mabao 3-1 na kufuzu kwa robo fainali.
Panama FC ikiwa nyumba Uwanja wa Uhuru imekubali kipigo cha mabao 5-2 kutoka kwa Sahare All Stars.
Ubora wa safu ya kiungo na ushambuliaji ya Sahare FC, umeifanya timu hiyo isonge mbele kwa kishindo katika hatua hiyo.
Panama ndio ilikuwa mwenyeji wa mchezo huo, ilipata changamoto ya kuzuia mashambulizi kila wakati ili isifungwe mabao mengi.
Katika mchezo mabao ya Sahare FC yalifungwa na Kassim Tiote aliyefunga mabao mawili huku Hussein Zola, Ally Salim na Issa Ubaya kila moja alifunga bao moja.
Tiote alisema alijitoa kwa nguvu na kutuliza akili kuhakikisha timu yake inasonga mbele kwenye michuano hiyo.
"Haikuwa safari rahisi kufika hatua hii,ushirikiano wa timu nzima ndio umetufanya tuibuke na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya wenyeji wetu Panama ingawa tumechezea Uwanja wa Uhuru ambao ni mgeni kwetu wote," amesema Tiote.